Msajili wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk. Benson Ndiege (kushoto), akibadilishana hati za makubaliano na Mkurugenzi wa Biashara wa Mixx, Bw. James Sumari, baada ya kuendeleza ushirikiano kati ya Mixx na TCDC wakati wa hafla iliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni. Ushirikiano huo unalenga kuimarisha huduma za kifedha kidijitali kwa vyama vya ushirika, kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa mamilioni ya wakulima nchini kupitia matumizi ya teknolojia.
………….
● Makubaliano yanalenga kuongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa vyama vya ushirika kupitia teknolojia.
Dodoma, Julai 5, 2026 – Mamilioni ya wakulima nchini wanatarajiwa kunufaika na huduma za kifedha kidijitali kufuatia muendelezo wa makubaliano ya ushirikiano kati ya kampuni ya Mixx na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC).
Makubaliano hayo yanalenga kuboresha usimamizi wa fedha kwa vyama vya ushirika, kuongeza uwazi na uwajibikaji, pamoja na kurahisisha huduma kwa wanachama.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter Msoffe, alisema Biashara zinazopita kwenye vyama vya Ushirika inaribia sh. trilioni 5-7 ambazo zinaingia kwenye uchumi wa nchi na kufanya vyama vya ushirika kuwa moja ya taasisi muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara wa Mixx, Ndugu James Sumari, alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kifedha kwa wakulima.
“Tunataka vyama vya ushirika viweze kusimamia fedha zao kwa uwazi na kuwafikishia wanachama huduma za kifedha kwa urahisi zaidi. Hii itasaidia kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya uchumi wa wananchi,” alisema Sumari.
Kupitia mfumo wa Mixx Kikoba, vyama vya ushirika vitaweza kusimamia michango, kufanya malipo, kununua hisa, kupokea gawio na kuomba mikopo kwa njia ya simu za mkononi.
Bwana Sumari aliongeza kuwa, mpaka sasa kupitia jukwaa la Mixx Kilimo, zaidi ya wakulima 300,000 tayari wamefikiwa na huduma za kifedha, huku zaidi ya shilingi bilioni 700 zikiwa zimepitishwa katika sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Naye, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, alisema matumizi ya teknolojia ni muhimu katika kuboresha sekta ya ushirika.
Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia ili kuongeza uwazi na ufanisi katika vyama vya ushirika. Ushirikiano huu utasaidia kuwajengea uwezo viongozi na wanachama kupata huduma bora za kifedha,” alisema Dkt. Ndiege.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza matumizi ya huduma rasmi za kifedha kwa wakulima na kuimarisha mchango wa sekta ya ushirika katika uchumi wa Taifa.
