Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile ametoa wito kwa Sekretarieti ya Maadili kuharakisha mchakato wa kubadili sheria ya Maadili ili iguse kada nyeti ambazo hazitambuliki kama viongozi kwenye Sheria ya Maadili.

Mhe. Kihenzile ametoa wito huo tarehe 6 Julai, 2026 alipotembelea Banda la Sekretarieti ya Maadili lililopo kwenye maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar-es-Salaam.

“Maadili nyie mnatakiwa kuharakisha mabadiliko hayo ya Sheria ili kuzifikia kada nyeti zote, kwani kuna watumishi ambao sio viongozi ila wako kwenye maamuzi nyeti kuliko mimi Mbunge, mfano pale Bandarini” Mhe. Kihenzile. 

Kwa upande wake mwananchi aliyetembelea Banda la Maadili Bw. Samson Alphonce Manyamama ametoa ushauri kwa Sekretarieti ya Maadili kuwafikia viongozi wote kuanzia ngazi ya kitongoji pamoja na viongozi wote wa taasisi binafsi na Serikali.

Bw. Manyama amesisitiza utoaji wa elimu ya Maadili kwa wananchi kuanzia chini ili wajue chombo chao kinafanyaje kazi, naamini tukifanya ivi uelewa na uwazi kuhusu maadili utaongezeka na Nchi yetu itabadilika. 

“Mfano mie nilikuwa sijui kama kuna Baraza la maadili ambalo linakaa kama Mahakama kwa viongozi waliokiuka Maadili, uko mtaani tumezoea mabaraza ya Ardhi tu” Samson Manyama.

Afisa Maadili, Bi. Grace Matunda amesema kwa sasa viongozi wanaolengwa ni wale ambao wametajwa kwenye Sheria ya Maadili ya 1995, aidha elimu ya Maadili kwa sasa Taasisi imeanza kutoa elimu kupitia mikutano ya vijiji kwa vijiji, shuleni somo la Maadili linafundishwa pamoja na kuanzisha klabu za maadili kuanzia ngazi ya Shule ya msingi hadi vyuoni.