Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa onyo kwa wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na wasimamizi wa mitandao ya kijamii akiwataka kutoruhusu majukwaa yao kutumika kusambaza maudhui ya uchochezi yanayoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Katambi alisema hatua za kisheria hazitachukuliwa dhidi ya waandaaji wa maudhui pekee, bali pia kwa vyombo vya habari au majukwaa yatakayoruhusu maudhui yanayokiuka sheria na Katiba ya nchi.

Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutoa taarifa zisizo na uthibitisho, hali inayoweza kusababisha mgawanyiko na kuvuruga amani ya nchi.

Katambi alisema historia inaonyesha kuwa katika baadhi ya mataifa, vyombo vya habari vilitumika kuchochea migogoro na hata mauaji ya halaiki, hivyo Tanzania haina budi kujifunza kutokana na uzoefu huo kwa kuhakikisha amani inaendelea kulindwa.

Alisisitiza kuwa hakuna mshindi katika vurugu au vita, akieleza kuwa bila amani hakuna usalama, maendeleo wala umoja wa taifa.

Waziri huyo aliwahakikishia Watanzania kuwa hali ya usalama nchini ni shwari na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kulinda nchi na raia wake.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa Tanzania ipo salama. Serikali haipangiwi tarehe, siku zote iko tayari. Tumejipanga na tunaendelea kujipanga,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba yeyote atakayehusika na vitendo vya uchochezi au vurugu atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Katambi pia aliwataka wazazi na walezi kuwalea vijana katika misingi ya maadili na kuwatahadharisha dhidi ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa “jinai hailipi na jinai haiozi,” hivyo wahusika watawajibishwa popote walipo.