Munir Shemweta, Kwimba
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema Wizara yake itaendelea kuhakikisha wamiliki wa ardhi wanapatiwa hati miliki ili kutatua na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Dkt. Akwilapo amesema hayo Julai 6, 2026 wilayani Kwimba mkoani Mwanza wakati wa hafla ya kukabidhi hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi wa Kijiji cha Solwe, Kata ya Nyabiti, ambapo jumla ya wananchi 527 walikabidhiwa hati hizo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Akwilapo amesema utoaji wa hati ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha usimamizi wa ardhi na kulinda haki za wananchi kumiliki ardhi yao kwa mujibu wa sheria.
“Wizara itaendelea kuwatumikia wananchi na kuhakikisha migogoro ya ardhi iliyopo inatatuliwa kwa kutoa hati, sambamba na kuwachukulia hatua wanaokiuka miongozo ya usimamizi bora wa ardhi nchini,” amesema.
Aidha, Waziri Akwilapo amesema Wizara imejipanga kuhakikisha watumishi wake wanafanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na weledi, huku akiwahimiza wananchi kutoa taarifa dhidi ya watumishi watakaobainika kukiuka maadili ya utumishi wa umma.
“Tunataka watumishi wanyooke na watoe huduma bora kwa kuwa Serikali imewasomesha ili wawahudumie wananchi. Sisi kama Serikali tutasimamia hilo, lakini wananchi pia mtusaidie kwa kufuata na kutekeleza miongozo tunayotoa ili tutoke katika janga hili la migogoro ya ardhi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Bw. Ngwilabuzu Ludigija amesema suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi ni kuhakikisha wananchi wanapimiwa ardhi na kumilikishwa rasmi kupitia hati za ardhi.
Amesema wananchi wanapokuwa na nyaraka halali za umiliki, viongozi wa Serikali hupata msingi wa kisheria wa kusimamia na kutatua migogoro kwa ufanisi.
Naye Kamishna wa Ardhi nchini, Nathaniel Nhonge, ameishukuru sekta binafsi kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa zoezi la upimaji na umilikishaji wa ardhi, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kukamilisha mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 1,492 kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Wilson Luge amesema ofisi yake imejipanga kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Mwanza kuhakikisha ardhi inapangwa, inapimwa na wananchi wanamilikishwa, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo yamekuwa nyuma katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Zoezi la kukabidhi hati hati za hakimiliki za kimila kwa wananchi linafuatia kukamilika kwa kazi ya upimaji iliyofanywa kwa ushirikiano na mdau kampuni ya GSM Geo Tech Consultancy katika Kijiji cha Solwe wilayani Kwimba.

