Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam 

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati naMaji (EWURA CCC) limewataka wananchi kutumia huduma za umeme, maji, mafuta na gesi ya kupikia kwa kuzingatia taratibu na ushauri wa kitaalamu ili kupunguza gharama zisizo za lazima, kuimarisha usalama na kulinda haki zao kama watumiaji.

Wito huo umetolewa leo julai 06,2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), na Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji Mwandamizi wa EWURA CCC, Lugiko Lugiko, ambapo amesema wananchi wengi hupata hasara kutokana na ukosefu wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya huduma zinazodhibitiwa na EWURA.

Amesema matumizi ya mafundi wasio na sifa, vifaa duni vya umeme na kutofanya ukaguzi wa miundombinu ya ndani huchangia umeme kuvuja na kuongeza bili, huku pia yakiongeza hatari ya ajali za moto.

“Kila mtumiaji anapaswa kutumia fundi aliyesajiliwa na kuhakikisha mfumo wa umeme wa nyumba yake unakaguliwa mara kwa mara ili kuondoa hitilafu zinazoweza kusababisha matumizi makubwa ya umeme,” amesema.

Kuhusu huduma za maji, Lugiko amesema watumiaji wanapaswa kuhakiki usomaji wa mita na kuchunguza uwepo wa mivujo kwenye mabomba kabla ya kuhitimisha kuwa bili kubwa imetokana na makosa ya mamlaka za maji.

Aidha, amewataka watumiaji wa gesi ya kupikia kusafirisha mitungi ikiwa imesimama na kuihifadhi sehemu zenye hewa ya kutosha ili kupunguza hatari ya uvujaji wa gesi na milipuko ya moto.

Kwa upande wa mafuta, amewasisitiza madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha pampu zinaanza kusoma sifuri kabla ya kujaziwa mafuta na kudai risiti kila wanapofanya malipo, akieleza kuwa risiti ndiyo nyaraka muhimu ya kufuatilia malalamiko endapo kutatokea hitilafu kwenye mafuta yaliyonunuliwa.

Lugiko pia amesema EWURA huendelea kutangaza bei kikomo za mafuta kila Jumatano ya kwanza ya mwezi ili kuwawezesha wananchi kufahamu bei halali na kujiepusha na udanganyifu.

Akizungumzia matumizi ya nishati safi ya kupikia, amesema EWURA CCC inaunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034, akibainisha kuwa majiko ya kisasa ya umeme ni salama, yanatumia umeme kidogo na yanasaidia kupunguza gharama za kupikia pamoja na kulinda mazingira.