Maadhimisho ya 5 ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU), yanayofanyika tarehe 5 hadi 7 Julai 2026, yamefunguliwa rasmi Nchini Burundi ikiwa ni hatua muhimu ya kihistoria ya kuendeleza lugha ya Kiswahili, yakifanyika sambamba na Kongamano la 3 la Kimataifa la Kiswahili kupitia Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), yakiwakutanisha wadau wa Kiswahili kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwingineko duniani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo, Waziri wa Vijana, Michezo na Utamaduni wa Jamhuri ya Burundi, Bi. Lydia Nsekela, amesisitiza kuwa Kiswahili ni nyenzo muhimu ya kuimarisha mshikamano wa kikanda, kukuza utamaduni na kuendeleza ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika Mashariki. Aliongeza kuwa serikali ya Burundi itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza na kueneza matumizi ya Kiswahili katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, utamaduni na teknolojia.
Maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Kiswahili, Wingi-Lugha, na Akili Unde (Kiswahili, Multilingualism and Artificial Intelligence)”, ambapo washiriki wanashiriki mijadala ya kitaaluma, mawasilisho ya mada mbalimbali pamoja na maonesho ya teknolojia yanayoonesha nafasi ya Akili Unde katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Kongamano hilo linafanyika likilenga kutoa mapendekezo yatakayochochea matumizi ya Kiswahili katika elimu, utafiti, ubunifu wa kidijitali na ushirikiano wa kimataifa.
kilele cha maadhimisho hayo ni julai 7 , 2026, ambapo shughuli rasmi zitahitimishwa kama sehemu ya kuendeleza ajenda ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kimataifa inayochochea maendeleo na umoja wa Afrika Mashariki.

