
Mkuu wa Idara ya Udahili wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Michael Mangula akizungumza na mwandishi wetu katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026.
……..
Chuo Kikuu Mzumbe kimesema kimejipanga kuendelea kuisaidia jamii kwa kutoa elimu bora inayozalisha wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi, pamoja na kujiajiri kupitia taaluma mbalimbali za ubobezi zinazotolewa na chuo hicho.
Akizungumza na mwandishi wetu katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, Mkuu wa Idara ya Udahili wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Michael Mangula, amesema dirisha la udahili kwa ngazi za Diploma, Shahada za Uzamili (Master’s) na Uzamivu (PhD) tayari limefunguliwa na litafungwa Oktoba 2026.
Ameongeza kuwa udahili wa ngazi ya Shahada ya Kwanza (Degree) utafunguliwa rasmi Julai 15, 2026, kwa kuzingatia kalenda ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Dkt. Mangula amesema chuo hicho kinatoa mafunzo katika fani mbalimbali zikiwemo Uhasibu na Fedha, Uongozi na Utawala, Mazingira, Sheria, Biashara na Ujasiriamali, Uchumi, Sayansi na Teknolojia, Ualimu, Utawala wa Sekta ya Afya pamoja na Usimamizi wa Miradi ya Afya.
“Ukifika katika banda letu tunatoa huduma ya udahili bure, sambamba na kuwashauri wanafunzi kuhusu fani zinazowafaa kulingana na ufaulu wao wa masomo,” amesema Dkt. Mangula.
Aidha, amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinatarajia kufungua kampasi mpya mkoani Tanga ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa chuo hicho kinaendelea kutekeleza kaulimbiu yake isemayo, “Chuo Kikuu Mzumbe: Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.”
