📍
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameipongeza SELF Microfinance Fund kwa mchango wake katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo, bima na elimu ya fedha huku akisema huduma hizo zimeendelea kuongeza ujumuishi wa kifedha na kufungua fursa za maendeleo kwa makundi mbalimbali nchini.
SELF Microfinance Fund ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha inayotoa mikopo, bima na elimu ya fedha kwa lengo la kuwawezesha wananchi, hususan wenye kipato cha chini, kuanzisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Balozi Omar ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la SELF katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, leo Julai 2, 2026, ambapo ameeleza kuwa mfuko huo unatekeleza kwa ufanisi dhamira ya Serikali ya kuwafikishia wananchi huduma za kifedha zinazochochea maendeleo ya kiuchumi.
Amesema elimu ya fedha inayotolewa sambamba na mikopo na huduma za bima imekuwa nyenzo muhimu inayowasaidia wananchi kutumia vyema fursa za uwekezaji, uzalishaji na biashara.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa SELF Microfinance Fund, Petro Mattaba, amesema taasisi hiyo hutoa mikopo kupitia taasisi za huduma ndogo za fedha pamoja na mikopo ya moja kwa moja kwa wananchi.
Amefafanua kuwa mfumo wa kutoa mikopo kupitia taasisi hizo unasaidia kuwafikia wananchi waliopo katika maeneo ambayo SELF haina huduma za moja kwa moja, hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.
Mattaba amesema walengwa wa mikopo ya moja kwa moja ni watumishi wa umma, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima, wafugaji na wavuvi, ambao hupata mitaji ya kuendeleza na kupanua shughuli zao za uzalishaji na biashara.
Aidha, amesema SELF kwa sasa ina matawi 12 Tanzania Bara na tawi moja Zanzibar, hali inayorahisisha wananchi kupata huduma za mikopo, bima pamoja na ushauri wa kifedha karibu na maeneo yao.
“Tumeshiriki Maonesho ya Sabasaba ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SELF, ikiwemo mikopo, bima na elimu ya fedha, ili waweze kuzitumia fursa hizo kuboresha maisha yao na kukuza shughuli zao za kiuchumi,” amesema Mattaba.
Ameongeza kuwa SELF inaendelea kushiriki katika utekelezaji wa programu mbalimbali za Serikali zinazolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi, zikiwemo programu za mikopo kwa vijana, wanawake na makundi mengine maalumu.
Kwa mujibu wa Mattaba, mwaka 2025 mfuko huo ulitoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 43 iliyowanufaisha wananchi zaidi ya 38,000, huku zaidi ya asilimia 51 ya wanufaika wakiwa wanawake.
Amesema pia SELF inaendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa taasisi za huduma ndogo za fedha ili kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wengi zaidi, hususan waishio vijijini na maeneo yenye huduma chache za kifedha.
Mattaba amewahimiza wananchi kutembelea banda la SELF katika Maonesho ya Sabasaba ili kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo na kupata taarifa za fursa mbalimbali za mikopo zinazoweza kuwasaidia kuinua uchumi wa familia na biashara zao.
