NA: DK. REUBENI LUMBAGALA 

Malezi bora ya watoto yanapaswa kutiliwa mkazo ili kujenga jamii yenye watu wenye maadili, nidhamu, uzalendo na uwajibikaji katika maisha yao.

Wazazi wamepata baraka ya kupata watoto kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Watoto hao wanapaswa kuendelea kuwa baraka kwa kuhakikisha wanapata malezi na matunzo muhimu.

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na kulegalega malezi ya watoto. Baadhi ya wazazi na walezi ambao ndiyo wadau wa kwanza wa kusimamia malezi ya watoto wamekuwa walipambana na matunzo ya watoto huku wakisahau malezi yao.

Wazazi na walezi wanahangaika kutafuta fedha za kuwapatia watoto wao mahitaji muhimu kama vyakula, mavazi, mahitaji ya shule ili wafurahie maisha. Hili ni jambo zuri na la kupongezwa na kila mtu.

Changamoto inayokuja ni pale wazazi na walezi wanapojitahidi kutoa matunzo na kusahau suala la malezi ambalo ni la muhimu sana.

Julai 02, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani alitoa somo zuri la malezi kwa wazazi na walezi. 

Ni kwamba, Dk. Buriani alitoa somo hilo alipomwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, katika kilele cha Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika na Kampeni ya Kitaifa ya Maadili na Malezi Chanya Kwa Watoto yenye kaulimbiu isemayo “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara”.

Katika hafla hiyo, Balozi Dk. Buriani alisema, “Wazazi wanatakiwa kutenga muda kuwafuatilia watoto, kuwapa malezi bora, malezi si hiari bali ni wajibu kwa wazazi na walezi”.

Kimsingi, Dk. Buriani alihimiza juu ya wazazi na walezi kutenga muda wa kufuatilia watoto wao na kuwalea watoto kwa misingi ya imani za dini zao.

Hivyo basi, wazazi na walezi wazingatie ushauri huu chanya uliotolewa. Wazungumze na watoto wao kutambua changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa ustawi wao. Pia, wafuatilie maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao shuleni ili wafanye vizuri zaidi katika masomo yao.

Sanjari na hilo, wazazi na walezi wasimamie suala la mafundisho ya dini kwa watoto wao ili wawe na hofu ya Mungu na mwenendo mwema unaokubalika katika jamii na mbele za Mungu.

Naamini, haya yakifanyiwa kazi, tutajenga kizazi chenye maadili mazuri ambayo ni chachu ya maendeleo kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla, na hili litafanya hata utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 kuwa rahisi.

Maoni: 0620 800 462.