Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imeweka mkakati wa miaka 50 ijayo wa kuhakikisha masoko yanatengenezwa kabla ya bidhaa kuzalishwa, ikiwa ni sehemu ya kuendana na mwelekeo wa dunia wa kuzalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya soko.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yaliyofanyika Julai 3, 2026 jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kapinga amesema Tanzania imejijengea hadhi mpya katika biashara ya kimataifa kupitia Diplomasia ya Uchumi, hatua iliyosaidia kufungua masoko mapya, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na mataifa mbalimbali, kuongeza imani kwa wawekezaji na kuiweka nchi katika nafasi nzuri kwenye minyororo ya biashara ya kikanda na kimataifa.

“Miaka 50 iliyopita TANTRADE ilikuwa na jukumu la kuitangaza Tanzania, lakini kwa miaka 50 ijayo imejipanga kuhakikisha inatengeneza masoko kabla bidhaa hazijazalishwa. Dunia ya leo haiuzi bidhaa zilizozalishwa, bali huzalisha bidhaa zinazohitajika na soko. Huo ndio mwelekeo tunaoutazamia,” amesema Mhe. Kapinga.

Ameeleza kuwa takwimu za mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi zinaonesha wazi kuwa Tanzania haiuzi bidhaa pekee, bali pia thamani, ubora na ushindani. Kutokana na hali hiyo, Wizara imejipanga kuhakikisha maonesho ya Sabasaba yanakuwa jukwaa linalochochea ushindani wa viwanda vya ndani, kupanua fursa za mauzo ya nje na kuunganisha sekta binafsi ya Tanzania na minyororo ya thamani ya kikanda na kimataifa.

Aidha, amesema Serikali inalenga kuyafanya maonesho hayo kuwa sehemu muhimu ambapo biashara hukutana na teknolojia, uwekezaji hukutana na ubunifu, na sera hukutana na fursa za masoko kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya biashara nchini.

Amesisitiza kuwa jukwaa hilo litawasaidia wazalishaji kupata taarifa za masoko kwa wakati, kuwaunganisha na wanunuzi wa kimataifa, kuvutia uwekezaji wenye tija na kuongeza mauzo ya bidhaa zenye thamani kubwa zinazobeba chapa ya “Made in Tanzania.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Shariff Ali Shariff, amesema Zanzibar inaendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma, pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi.

Amesema juhudi hizo zinaenda sambamba na azma ya kujenga uchumi shindani unaotegemea uzalishaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa.

“Tunawapongeza washiriki wote wa maonesho haya kwa kuendelea kutumia jukwaa hili kutangaza bidhaa, huduma na fursa mbalimbali za biashara. Tunawahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika soko la ndani, Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, Eneo Huru la Biashara la Afrika pamoja na masoko ya kimataifa,” amesema Mhe. Shariff.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Dkt. Latifa Mohamed Khamis, amesema katika kipindi cha miaka 50, maonesho hayo yamezalisha fursa za biashara zenye thamani ya takriban shilingi trilioni 129.21, hatua iliyochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya biashara duniani.

Amesema katika kipindi hicho, jumla ya nchi 54 zimeshiriki mara 564, huku zaidi ya watu milioni 10.08 wakitembelea maonesho hayo, kampuni zaidi ya 38,059 zikishiriki na zaidi ya ajira 631,900 kuzalishwa.

“Kwa mwaka huu tunatarajia kufikia mikataba na mauzo ya papo kwa papo yenye thamani ya wastani wa shilingi bilioni 17, biashara zaidi ya 3,752 kupitia waonyeshaji 4,800, watembeleaji 624,380 pamoja na ajira mpya zaidi ya 26,000,” amesema Dkt. Latifa.