NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
DIWANI wa Kata ya Miono ,Halmashauri ya Chalinze ,Bagamoyo Mkoa wa Pwani Juma Mpwimbwi, amelalamikia mifugo holela ikiwa ni pamoja na inayomilikiwa na mfugaji , aliyemtaja kwa jina la Malimengi,ambayo inasababisha kundi la wakulima kupata hasara ya kilimo chao kutokana na uharibifu.
Mbele ya Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani hapa chini ya Mwenyekiti wake Alhaj Abdul Sharifu, Mpwimbwi alisema ,mfugaji huyo amekuwa na kiburi cha fedha alizonazo, hali inayowaweka wananchi kwenye sintofahamu kubwa.
“Naiomba Kamati itoe tamko lenye tija, kwani juhudi zao zinaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mifugo inayoingia kwenye mashamba yao, na wanapotoa taarifa kwenye mamlaka husika hakuna hatua zinazochukuliwa,” alibainisha Mpwimbwi.
“Sisi Wazigua hatujawahi kulia njaa kwa kukosa chakula, lakini mwaka huu wana-Miono wanahofu ya kukabiliwa na njaa kutokana na wingi wa mifugo maeneo ya mijini sanjali na mashambani hivyo kiathiri kwa kiasi kilubwa mazao,” alisema Mpwimbwi.
Mmoja wa wakulima akijitambulisha kwa jina la Hemed Mningo, alisema jamii ya wafugaji wanasababisha migogoro kutokana na mifugo yao kuingia kwenye mashamba.
“Hii mifugo unayoiona kwenye zizi hapa ofisi ya Kijiji, imekamatwa ikiwa ndani ya mashamba, hapa wanasubiliwa wamiliki wafike waende kwenye mashamba yakafanyiwe tathimini mazao yaliyoharibiwa, ili zianze taratibu za fidia,” alisema Mningo.
Msafara ukiwa Miono baada ya Diwani huyo kulalamika, Sharifu alifafanua watatoa tamko zito katika majumuisho ya ziara, kwenye kikao kitachojumuisha Wakurugenzi na wataalamu wa halmashauri ya Chalinze na Bagamoyo.