• Awataka wakuu wa mikoa kuendeleza kampeni za usafi

Na OWM – TAMISEMI, Arusha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki amewapongeza Maafisa Afya wa Mikoa na Halmashauri nchini kwa kupunguza mlipuko wa kipindupindu kutoka maambukizi ya watu 12,000 hadi 700 kwa mwaka 2025/26, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo waliyojiwekea mwaka jana.

Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo Juni 01, 2026 jijini Arusha, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathmini ya utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira nchini, unaofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa (AICC).

“Niwapongeze kwa utekelezaji wa lengo la kupunguza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mlilojiwekea mwaka jana, mmefanikiwa kupunguza kiwango cha mlipuko kutoka kesi 12,000 hadi 700, sasa niwaombe mwaka huu muweke lengo la kuendelea kutokomeza mlipuko wa ugonjwa huu,” amesema Prof. Shemdoe.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewasisitiza Wakuu wa Mikoa, Maafisa Afya wa Mikoa na Halmashauri kuwahimiza wananchi kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukizwa kama shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo, kiharusi, pumu, ambayo yanasababisha vifo na kuathiri nguvu kazi ya taifa.

Aidha, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuendelea na kampeni ya kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi kwani kampeni hiyo itaendelea kuimarisha hali ya usafi, kupunguza na kuondoa kabisa changamoto uwepo ya magonjwa ya milipuko ikiwepo kipindupindu.

Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo, kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na namna anavyowekeza katika sekta ya afya na mazingira, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maono yake ya kutaka kila mtanzania awe na afya bora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Makalla amemhakikishia Prof. Shemdoe kuwa, mkoa wake umejipanga ipasavyo katika utekelezaji wa miradi ya afya, na kuongeza kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na wataalam wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Prof. Tumaini Nagu amesema mkutano huo umelenga kutathmini mpango kazi wa mwaka 2025/26 waliojiwekea maafisa afisa afya kuanzia ngazi ya mikoa hadi Mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na kuandaa mpango kazi wa mwaka wa fedha 2026/27. 

Akifafanua malengo la mkutano huo, Mkurugenzi wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa, malengo ya mkutano huo ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa afua ya afya na usafi wa mazingira katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri kwa kuzingatia viashiria vya kitaifa na malengo ya kisekta.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Maafisa Afya wa Halmashauri Bw. Fanuel Nyadwike amemuahaidi Prof. Shemdoe kuwa, watatumia mkutano huo kutathmini utekelezaji wa shughuli za mwaka uliopita wa 2025/26, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuboresha huduma za afya na usafi wa mazingira kwa mwaka 2026/27. 

Mkutano huo wa mwaka huu wa 2026 umebeba kaulimbiu isemayo “Kuimarisha Mifumo Jumuishi na Endelevu ya Afya na Usafi wa Mazingira ili Kujenga Jamii Stahimilivu yenye Afya Bora”.