Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (kulia), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma za Next Generation Sequencing (NGS), hatua inayofungua enzi mpya ya tiba ya jenomiki nchini. Uzinduzi huo unakiweka Chuo Kikuu kuwa kitovu cha kitaifa na kikanda cha sayansi ya jenomiki, uchunguzi wa kisasa wa magonjwa, utafiti na ubunifu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza jambo wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) unaofanyika Julai 1, 2026 katika Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.

………..

Serikali imesisitiza umuhimu wa kufanya tafiti za kisayansi ili kuthibitisha usalama na ufanisi wa tiba za asili kabla ya kuziingiza rasmi katika mfumo wa huduma za afya nchini.

Akifungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) uliofanyika Julai 1, 2026 katika Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema hatua hiyo itasaidia kuziba pengo lililopo kati ya tiba za asili na tiba za kisasa.

Amesema tiba za asili zinazotumiwa na wananchi zinapaswa kufanyiwa tafiti, majaribio ya kitabibu na tathmini za kitaalamu ili ziweze kuthibitishwa kwa ushahidi wa kisayansi na kutumika kwa usalama.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, madai yote kuhusu uwezo wa tiba yoyote, ikiwemo tiba asili, yanapaswa kuthibitishwa kisayansi ili kubaini kiwango sahihi cha matumizi, usalama wake na aina ya wagonjwa wanaoweza kunufaika nayo.

“Lengo si kupinga tiba asili, bali kuhakikisha zinaboreshwa kupitia tafiti za kisayansi na kutumika kwa usalama ndani ya mfumo rasmi wa huduma za afya,” amesema.

Aidha, amesema Serikali imepanga kuandaa warsha za kitaifa zitakazowakutanisha watafiti, waganga wa tiba asili, wadhibiti pamoja na wataalamu wa haki miliki kwa lengo la kuweka mfumo wa kutathmini na kulinda maarifa ya tiba za asili.

Prof. Mkenda pia ameonya dhidi ya matumizi ya tiba zinazotegemea ushuhuda ambao haujathibitishwa kisayansi, akieleza kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za wagonjwa.

Amesisitiza kuwa majaribio ya kitabibu, uchunguzi wa maabara na tafiti za kina ni muhimu kabla ya tiba yoyote kuruhusiwa kutumika.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la MUHAS, Makata Yambi, amesema tafiti na ubunifu wa ndani vina mchango mkubwa katika kuimarisha mfumo wa afya, huku mkutano huo ukiwa jukwaa muhimu la watafiti, watunga sera na wadau wa maendeleo kubadilishana uzoefu na kujadili suluhisho za changamoto za afya.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema chuo kinaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa kama akili bandia (AI), genomiki na mbinu za kisasa za uchunguzi wa magonjwa ili kuongeza ubora wa tafiti na huduma za afya.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa huduma za uchunguzi wa kizazi kipya wa vinasaba (Next Generation Sequencing) kumeiwezesha MUHAS kuwa kitovu cha kikanda katika sayansi ya jenomu na tiba mahsusi, hatua itakayosaidia pia kutathmini kwa kina tiba zinazotokana na maarifa ya tiba asili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Prof. Raphael Sengeja, amesema mkutano wa mwaka huu umepokea tafiti 247, zikiwemo 138 za uwasilishaji wa moja kwa moja na 109 za mabango, zikihusu maeneo mbalimbali ikiwemo tiba asili, akili bandia, genomiki, afya ya uzazi, usugu wa vimelea dhidi ya dawa na uimarishaji wa mifumo ya afya.

Amesema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kutatua changamoto halisi za sekta ya afya na kuboresha ustawi wa wananchi, badala ya kubaki kwenye machapisho ya kitaaluma pekee.