Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amempa siku 14 mkandarasi anayejenga barabara ya Mbulu – Hydom kufikisha vifaa vyote vya ujenzi vinavyohitajika katika eneo la mradi kama mkataba unavyoeleza.
Ulega alitoa maagizo hayo wakati alipokuwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo kampuni ya Jiangxi Geo Engineering ya China inajenga kipande cha Labay – Hydom chenye urefu wa kilomita 25 kwa lami.
Wakati akitaka kupewa taarifa na mkandarasi, Waziri huyo alielezwa kwamba asilimia takribani asilimia 50 ya vifaa tayari viko eneo la tukio – taarifa ambayo Ulega alisema haikuwa ya ukweli kwa sababu nyaraka zinaonyesha ni asilimia 33 tu ya vifaa ndiyo vimefika katika eneo la mradi.
“Nyaraka zinaonyesha vifaa vilivyoko hapa ni asilimia 33 tu. Nakuagiza kwamba nataka kuona vifaa vyote vinavyohitajika vinafika hapa katika muda wa wiki mbili kutoka sasa. Hayo ndiyo masharti ya mkataba na ni muhimu yakafuatwa“ alisema Ulega.
Ulega alisema umuhimu wa kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kwa wakati ni kuwa uhakika wa mradi kukamilika kwa wakati pia unakuwa mkubwa na faida za ujenzi huo kuanza kuwafikia wananchi haraka.
Ulega alisema barabara hiyo ni ya muhimu kwa sababu ndiyo inaunganisha mikoa mitano ambayo ni Arusha, Manyara, Simiyu, Singida na Shinyanga na unatelelezwa kwa taratibu wa Sanifu Jenga (Design and Build).
Ulega ameendelea kuwasisitiza watendaji na wasimamizi wa mradi kusimamia ubora wa ujenzi wa barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.
“Haipendezi kuona barabara iliyojengwa ndani ya mwaka mmoja ina mashimo hiyo inatokana na kujengwa chini ya kiwango. Suala la ubora halina mjadala na sitalivumilia nitawachululia hatua kwa wote watakaoshidwa kusimamia hilo”, amesema Ulega.
Ulega ameongeza kuwa suala la ubora wa barabara halihitaji mjadala hivyo watendaji kusimamia na kukagua miradi wazingatie ubora na ufanisi katika kila hatua ya ujenzi wa barabara.

