Watendaji wa Chuo cha Maji wametakiwa kutekeleza majukumu kwa kuzingatia uwajibikaji wa pamoja na utawala bora ili kuleta tija katika Sekta ya Maji nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema hayo katika kikao kazi na Menejimenti ya Chuo cha Maji jijini Dar es salaam.
Amesema ni muhimu kwa menejimenti ya chuo kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja katika kutatua mambo mbalimbali yanayokikabili chuo bila kurushiana mpira.
“Chuo hiki kipo kutusaidia Sekta ya Maji kukabiliana na changamoto zinazotukabili kwa kutuzalishia wataalamu, naomba nisisitizie mitaala inayofundishwa kuendana na ukuaji wa teknolojia, na wanafunzi wakishirikishwa kwa vitendo katika miradi mbalimbali ya kmakakati inayoendelea nchini ili kuwajengea uwezo na ujuzi” Mhandisi Mwajuma amesema.
Ameongeza kuwa ni muhimu ubora wa elimu unaotolewa chuoni hapo kuzingatiwa kwa viwango kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Sekta ya Maji ikiwamo mamlaka za maji na RUWASA pamoja vyuo mbalimbali ili kuzalisha wataalamu wenye ubora mkubwa na watakao weza kufanya kazi katika Sekta mbalimbali.
“Nipende kusisitiza kila mtumishi wa Sekta ya Maji anatakiwa kuleta matokea chanya katika Taasisi yake, na huu ndio utawala bora na uwajibikaji, kama Wizara tutaendelea kuwa bega kwa bega na chuo huku tukitegemea mabadiliko makubwa chanya chuoni hapa” Mhandisi Mwajuma ameainisha.
Kwa upande wake Rekta wa Chuo cha Maji Dkt.Adam Karia ameeleza kuwa chuo kinaendelea kupiga hatua hususani katika udahili wa wanafunzi ambapo hadi sasa chuo kina wanafunzi zaidi ya 5,800 ambapo wanakijikita kuongeza kada mbalimbali kulingana na mahitaji ya Sekta ya Maji nchini. 
