Na Mwandishi Wetu,
Kampuni ya mawasiliano ya Halotel Tanzania imeingia kwa kishindo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama SabaSaba, ikiwa imeandaa uzoefu wa kipekee wa kidigitali kwa wageni wanaotembelea banda lake la maonesho.
Halotel imezindua rasmi ushiriki wake katika maonesho hayo yanayofanyika Dar es Salaam, huku ikibeba kauli mbiu ya “Teknolojia kutoka Moyoni” inayolenga kuonesha dhamira ya kampuni hiyo katika kuendeleza mageuzi ya kidigitali nchini Tanzania kupitia huduma bunifu za mawasiliano, kidigitali na kifedha.
Kupitia banda lake, Halotel imewaandalia wageni fursa ya kujionea huduma mbalimbali za kisasa ikiwemo teknolojia ya mtandao wa 5G, huduma ya intaneti ya kasi ya juu ya HaloFibre, suluhisho za kidigitali kwa wafanyabiashara pamoja na huduma za kifedha kupitia HaloPesa.
Huduma ya HaloPesa imeendelea kuwa sehemu muhimu ya maonesho hayo kwa kuwawezesha wateja kupata huduma salama na rahisi za kifedha kidigitali ikiwemo kutuma na kupokea fedha, kuweka na kutoa fedha pamoja na kufanya malipo mbalimbali kwa urahisi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo katika banda la Halotel, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Halotel Tanzania, Bw. Abdallah Salum, amesema SabaSaba ni jukwaa muhimu linaloiwezesha kampuni hiyo kuwasiliana moja kwa moja na wateja na kuonesha namna teknolojia inavyoweza kuboresha maisha ya wananchi.
“Saba Saba inatupatia jukwaa muhimu la kuwasiliana moja kwa moja na wateja wetu na kuonesha ubunifu unaoendelea kuboresha maisha yao kupitia teknolojia,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Halotel Tanzania, Bi. Tran Thi Thuy Dung, amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika suluhisho bunifu zitakazochochea maendeleo ya kidigitali nchini.
“Halotel inaendelea kujitolea kuwekeza katika suluhisho bunifu zinazoboresha uzoefu wa wateja na kuharakisha mageuzi ya kidigitali nchini Tanzania. Kupitia maonesho haya, tunawapa wageni nafasi ya kushuhudia kwa vitendo huduma zetu na kuona athari zake halisi katika maisha ya kila siku,” amesema.
Naye Meneja wa Masoko wa HaloPesa, Bi. Aidat Lwiza, amesema kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya HaloPesa, kampuni hiyo imeandaa ofa na shughuli mbalimbali kwa ajili ya kuwapa wateja uzoefu wa kipekee katika kipindi cha maonesho hayo.
“Kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya HaloPesa, tunafuraha kuleta ofa na uzoefu wa kipekee kwa wateja ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa huduma za kifedha kidigitali zilizo rahisi na zenye uhakika katika kipindi chote cha maonesho ya SabaSaba,” amesema.
Halotel imewaalika wananchi, wadau na washiriki wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kutembelea banda lake ili kujionea huduma mbalimbali za kiteknolojia pamoja na ofa maalum zitakazopatikana kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026.

