Jengo la Utawala katika shule mpya ya sekondari Luholosi Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma.

Moja ya vyumba vya madarasa katika shule ya Luholosi iliyojengwa na Serikali ili kuwaondolea watoto wa kijiji cha Langiro asili kwenda maeneo mengine kufuata masomo ya sekondari
……………
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
ADHA ya kutembea umbali mrefu kwa watoto wanaomaliza darasa la saba katika kijiji cha Langiro Asili kata ya Langiro ambao wanachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za sekondari zilizopo kata nyingine imekuwa historia,ni baada ya Serikali kutoa zaidi ya Sh.milioni 500 kujenga shule mpya ya sekondari ya Luholosi.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Joseph Kashushura alisema,fedha hizo zimetoka Serikali kuu kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya sekondari nchini(SEQUIP).
Alisema,lengo la kujenga shule hiyo ni kuwasaidia watoto wanaotoka katika kijiji hicho na vijiji vya jirani waweze kusoma karibu na maeneo yao ili kuwaondolea usumbufu kwenda vijijini vingine kufuata masomo na kuboresha taaluma.
“Katika kata ya Langiro kuna uhitaji mkubwa wa watoto kusoma,ndiyo maana Serikali kwa kutambua changamoto iliyopo imetoa fedha kwa ajili ya kujenga shule hiyo ambayo imesajiriwa na watoto wameanza kusoma ujenzi wa miundombinu mingine unaendelea”alisema Kashushura.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi ambazo zinasaidia kutoa na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi.
Kwa upande wake mhandisi wa Halmashauri hiyo Neema Mbilinyi alisema,walipokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo kumi ikiwemo jengo la utawala,madarasa manane na ofisi mbili za walimu, vyumba viwili vya maabara,jengo la TEHAMA,jengo la maktaba na nyumba moja ya mwalimu.
Aidha alisema,mpaka sasa majengo sita kati ya nane yamekamilika ambayo ni jengo la utawala,vyumba vinane vya madarasa,ofisi mbili za walimu pamoja na vyoo vya wavulana na wasichana.
Kwa mujibu wa Mbilinyi,kwa sasa kazi zinazoendelea kufanyika ni ujenzi wa maabara ya kemia na bailojia,maktaba na chumba maalum cha kompyuta na malengo ni kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyobaki ifikapo mwazi Julai mwaka huu.
Makamu mkuu wa shule hiyo Balo Seleman alisema,uwepo wa shule ya sekondari Luholosi una faida kubwa kwa sababu watoto wanaomaliza darasa la saba kutoka shule ya msingi Hagati na Lingomba na Mbula wanaochaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata masomo lakini kujengwa kwa shule hiyo ni faraja kwao.
“Mwanzo walikuwa wanatembea umbali mrefu hadi shule ya sekondari Mkoha kufuata masomo,tunamshukuru sana Mkurugenzi Joseph Kashushura kufanikisha ujenzi wa shule hii kwani watoto wanapata elimu bora pamoja na kuwaondolea usumbufu wa kwenda shule nyingin”alisema.
Mkazi wa kijiji hicho Yuda Ndunguru,ameipongeza Serikali na Halmashauri ya wilaya Mbinga kwa uamuzi wa kujenga shule hiyo ambayo imesaidia sana kumaliza changamoto kwa watoto wao ambao awali walikuwa wanakwenda kata nyingine kufuata masomo.
