Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 27 Juni, 2026 amehitimisha rasmi mafunzo ya mwaka mmoja ya Kozi ya Ukamanda na Unadhimu katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania, yaliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Duluti, mkoani Arusha.
Mahafali hayo, ambayo Dkt. Nyansaho alikuwa Mgeni Rasmi, yalihusisha jumla ya maafisa wahitimu 82 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na maafisa kutoka nchi mbalimbali rafiki. Mbali na kuhitimu Kozi ya Ukamanda na Unadhimu, wahitimu hao pia walitunukiwa Shahada za Umahiri na Stashahada katika Masuala ya Ulinzi na Usalama. Mafunzo hayo yalitolewa sambamba na kozi hiyo kwa lengo la kuwawezesha kupata maarifa ya kina kuhusu masuala ya ulinzi, usalama na uongozi wa kimkakati.
Akizungumza katika mahafali hayo, Waziri wa Ulinzi na JKT aliwapongeza wahitimu kwa mafanikio yao, akieleza kuwa kuhitimu kozi hiyo ni ushahidi wa bidii, nidhamu, ujasiri, uthabiti na kujitolea kwao katika kipindi chote cha mafunzo.
Alibainisha kuwa kozi hiyo ni miongoni mwa mafunzo ya kijeshi yanayotambulika kimataifa, hivyo wahitimu wanapaswa kujivunia mafanikio hayo makubwa.
“Mmethibitisha uwezo wa kukabiliana na changamoto za mafunzo makali na mmeonesha sifa za uongozi zinazohitajika kwa viongozi wa kijeshi wa sasa na wa baadaye. Mafanikio haya ni hatua muhimu katika safari yenu ya uongozi na utumishi kwa mataifa yenu,” alisema Dkt. Nyansaho.
Aidha, Waziri huyo aliushukuru uongozi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu chini ya Mkuu wa Chuo hicho, Meja Jenerali Stephen Mnkande, kwa maandalizi mazuri ya mafunzo hayo na kwa kumpa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 40 ya chuo hicho.
Katika hotuba yake, Dkt. Nyansaho alisisitiza kuwa majeshi ya ulinzi yanaendelea kuwa alama ya umoja wa kitaifa, uhuru na mshikamano wa mataifa.
Alieleza kuwa pamoja na jukumu la msingi la kulinda mipaka na mamlaka ya nchi, majeshi ya ulinzi yameendelea kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na maafa, kujenga miundombinu, kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa pamoja na kushiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani.

