*Lengo ni kuvikagua, kuviboresha na kuvitangaza kuelekea AFCON 2027

*Mkurugenzi wa Malikale azitaka taasisi chini ya Wizara kunadi kwa pamoja vivutio hivyo

Na Neema Chalila Mbuja, Dar es Salaam

MENEJIMENTI ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wakuu wa taasisi za Wizara leo Juni 27, 2026 wamefanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Makumbusho na Malikale ili kuona namna ya kuviboresha na kuvitangaza kuelekea Fainali za Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON – 2027) kwa lengo la kuwavutia na kuwahamasisha watalii kutembelea maeneo hayo.

Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Makumbusho ya Taifa, Makumbusho ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na Nyumba aliyoishi marehemu Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere wakati wa kupigania Uhuru wa Tanganyika eneo la Magomeni.

Maeneo mengine ni Jengo la Old Boma lililojengwa na Sultan miaka ya 1860 na Kituo cha Urithi wa Ukombozi Kusini mwa Afrika.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Malikale, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Cristowaja Ntandu amesema kuwa Idara ya Malikale ina vivutio vingi vinavyopaswa kuboreshwa na kutangazwa ili kuvutia wageni hususani kuelekea kipindi cha Michuano ya AFCON na kulitaka Shirika la Makumbusho ya Taifa (NMT) kuweka mkakati wa kina kutangaza maeneo ya Malikale.

Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zilizopo chini ya Wizara zimepewa jukumu la kuhifadhi na kuendeleza mikusanyo ya mali kale kwa ajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.