WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoahidiwa katika Mkoa wa Singida, ikiwemo barabara, reli ya kisasa (SGR), uwanja wa ndege pamoja na miradi ya maji, afya na elimu kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 27, 2026) alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Maonesho wa Mandewa, wilayani Ikungi, mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtuma kuwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Singida kuwa miradi yote ya maendeleo iliyoahidiwa itaendelea kutekelezwa hatua kwa hatua kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali.

“Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie kwamba mambo ambayo wabunge wenu wamekuwa wakiyasema na ambayo aliwaahidi wananchi wa Singida yatakwenda kutekelezwa,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya barabara ikiwemo Sabasaba–Sepuka–Ndago–Kizaga, Njia Panda–Makiungu–Mungaa–Misughaa–Ndago, Mkiwa–Itigi–Rungwa–Makongorosi, Iguguno–Nduguti–Sibiti, pamoja na Singida–Ilongero–Haydom, hatua zitakazorahisisha usafirishaji, biashara na kufungua fursa zaidi za kiuchumi katika Mkoa wa Singida na maeneo jirani.

Aidha, amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa reli ya kisasa (SGR) itakayofika Singida pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa utakaohudumia ndege za ukubwa mbalimbali na kuongeza fursa za uwekezaji na biashara.

Waziri Mkuu amesema kuchelewa kwa baadhi ya miradi kulitokana na uamuzi wa Serikali kuelekeza rasilimali katika kukamilisha miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Kigongo–Busisi, ambayo sasa imeanza kutoa manufaa makubwa kwa Taifa.

“Tulifanya uamuzi wa kufunga mkanda ili tukamilishe miradi ya kimkakati. Leo Tanzania ina ziada ya umeme na miradi hiyo imeendelea kutoa manufaa makubwa kwa wananchi na uchumi wa Taifa,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za maji, afya, elimu na miundombinu mingine ya kijamii sambamba na utekelezaji wa miradi hiyo ili kuongeza ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.