DODOMA, 27 Juni 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma imefanya Matembezi ya Hisani pamoja na Bonanza la Michezo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na maandalizi kuelekea Tuzo za Mheshimiwa Rais kwa Walipakodi.

Shughuli hizo zimewakutanisha watumishi wa TRA, walipakodi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha mshikamano, kuendeleza mahusiano mazuri na kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya Taifa.

Matembezi hayo ya hisani yalianzia katika Ofisi za TRA Mkoa wa Dodoma na kuhitimishwa katika Uwanja wa Kilimani, yakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Dkt. Sophia Kizigo, pamoja na Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Bw. Pendolake Elinisafi.

Baada ya matembezi hayo, washiriki waliendelea na bonanza la michezo lililoshirikisha watumishi wa TRA, walipakodi na wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Bw. Pendolake Elinisafi, alitoa historia fupi ya TRA tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 hadi kutimiza miaka 30 mwaka 2026.

Alieleza kuwa katika kipindi hicho TRA imepata mafanikio mbalimbali, ikiwemo maboresho makubwa ya mifumo ya utoaji huduma kwa walipakodi, matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa mapato na kuimarika kwa uhusiano kati ya TRA na walipakodi.

Alisema maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Miaka 30 ya TRA, Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea kwa Taifa Letu.”

Alibainisha kuwa TRA Dodoma imeadhimisha miaka hiyo kwa kutekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo kurejesha kwa jamii kupitia miradi ya kijamii, kupanda miti katika Shule ya Sekondari Miuji pamoja na kuandaa matembezi ya hisani na bonanza la michezo lililowashirikisha walipakodi na wananchi.

Aliongeza kuwa shughuli hizo zimeendelea kuimarisha uaminifu, ukaribu na ushirikiano kati ya TRA na walipakodi, jambo linalochochea ulipaji wa kodi kwa hiari na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, mgeni rasmi, Mhe. Dkt. Sophia Kizigo, aliipongeza TRA kwa kazi kubwa ya ukusanyaji wa mapato kwa uadilifu na kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa kwa walipakodi.

Pia alimpongeza Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Bw. Pendolake Elinisafi, kwa uongozi wake unaoendelea kuimarisha utulivu katika ukusanyaji wa mapato na kujenga mazingira rafiki kwa walipakodi kwa kusikiliza na kutatua changamoto zao, si katika Jiji la Dodoma pekee bali pia katika wilaya zote za mkoa huo.

Aidha, alisema ushirikiano mzuri unaoendelezwa kati ya TRA, walipakodi na jamii kupitia shughuli za kijamii na michezo unaimarisha uelewa wa umuhimu wa kulipa kodi na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi hiyo.

Akihitimisha, Mhe. Dkt. Sophia Kizigo aliishukuru TRA kwa mwaliko huo na kwa kuendelea kuonesha dhamira ya kurudisha kwa jamii.

Aliwataka watumishi wa TRA kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu, huku akiwahimiza walipakodi kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, akisisitiza kuwa kodi ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa Taifa.