Na Mwandishi Wetu
Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Magereza, Balozi Phaustine Martin Kasike, ameagwa rasmi katika hafla iliyowakutanisha viongozi wa Serikali, Jeshi la Magereza, maafisa, askari na wadau mbalimbali, walioungana kumpongeza na kumshukuru kwa utumishi wake wa muda mrefu uliogusa maisha ya watu wengi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya chuo cha urekebishaji Tanzania TCTA Ukonga, washiriki walimuelezea Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Magereza Balozi Kasike kuwa ni kiongozi aliyeiongoza taasisi hiyo kwa uadilifu, weledi, nidhamu na uzalendo wa hali ya juu, huku akijenga misingi imara ya utendaji kazi na kuacha alama isiyofutika ndani ya Jeshi la Magereza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, alisema Balozi Kasike ametumikia taifa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, jambo lililomfanya kuwa kiongozi anayeheshimika na kuthaminiwa na watu wa kada mbalimbali.
Alisema historia ya Balozi Kasike inatoa funzo kuwa uaminifu, nidhamu, kujituma na uzalendo ni nguzo muhimu za mafanikio katika utumishi wa umma na kwamba Serikali itaendelea kuthamini mchango wake mkubwa.
Gugu pia alimwomba Balozi Kasike kuendelea kuwa karibu na Serikali na Jeshi la Magereza kwa kutoa ushauri na busara zake kila itakapohitajika, kutokana na uzoefu mkubwa alioupata katika kipindi chake cha utumishi.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, alisema Balozi Kasike amelitumikia Jeshi la Magereza kwa zaidi ya miaka 36 kwa uaminifu na kujituma, huku akitoa mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo.
Kamishna wa Jeshi la Magereza CGP Katungu alisema Balozi Kasike ameacha urithi mkubwa wa uongozi bora na misingi imara ambayo viongozi, maafisa na askari wa Jeshi la Magereza wataendelea kuienzi na kuikuza kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Katika hafla hiyo, askari na maafisa wa Jeshi la Magereza walitoa ushairi maalumu wakieleza sifa na mchango wa Balozi Kasike, wakisema ameacha alama kubwa katika taasisi hiyo na kwamba wataendelea kumkumbuka kwa maono na uongozi wake.
Walimshukuru kwa mchango wake mkubwa na kuahidi kuendeleza yale yote mema aliyoyaasisi, huku wakimuomba kuendelea kuwapa ushauri na hekima zake kila watakapohitaji mwongozo.
Awali, Balozi Kasike alikagua gwaride maalumu la heshima na kuagana na maafisa na askari wa Jeshi la Magereza, akihitimisha safari ya zaidi ya miongo mitatu ya utumishi uliotukuka, ulioacha historia ya uadilifu, uzalendo na uongozi wa mfano katika utumishi wa umma nchini.
Akitoa salamu zake kwa maafisa na askari wa Jeshi la Magereza Kamishna Mstaafu Balozi Kasike ameishukuru serikali na kwa kumuamini na Kumpa nafasi ya kuitumikia katika nyadhifa mbalimbali na kwamba ataendelea kuwa mfano na kioo kwa jamii katika kuishi maisha ya nidhamu uadilifu hata akiwa nje ya Jeshi la magereza na utumishi wa umma.
Amewashukuru maafisa wote wa jeshi na kuwaomba radhi endapo kama walikoseana wakati wa kztekeleza majukumu yao na yuko tayari kuendelea kutoa mchango wake pindi utakapohitajika
Kamishna mstaafu wa Jeshi la Magereza Balozi kasike alistaafu rasmi kwa mujibu wa sheria mnamo desemba mwaka jana.

