*Yatoa mwaka mmoja ili waweze kujiimarisha

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imetoa msamaha wa kodi ya mapato kwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa wafanyabiashara wadogo ambao ni wapya ili waweze kujiimarisha katika biashara wanazozianzisha.

“Ili kuwavutia wajasiriamali, Serikali itatoa msamaha wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wadogo ambao ni wapya kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe ya kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi,” amesema. 

Amesema hatua hiyo itawawezesha akinamama lishe na baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji, mafundi seremala na wachomeleaji na wengine wenye shughuli ndogondogo kuanzisha biashara zao bila kuwa na changamoto ya kudaiwa kodi ndani ya mwaka mmoja, na kwamba muda huo utatoa fursa ya kujiimarisha katika biashara wanazozianzisha.

Ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo (Ijumaa, Juni 26, 2026) wakati akielezea maeneo yaliyofanyiwa maboresho ya kodi katika hotuba ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Agosti 25, mwaka huu.

Akielezea eneo jingine ambalo limewekewa nafuu ya kikodi, Waziri Mkuu amesema Serikali itasamehe kodi kwenye vifaa vitakavyotumika katika vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme na kupunguza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10. Aidha, amewataka wadau wa sekta binafsi watumie fursa hiyo kuagiza mashine na vipuri vitakavyotumika kwenye vituo hivyo.

Akielezea azma ya Serikali kuimarisha mtiririko wa fedha katika mifuko ya miradi ya maendeleo, Dkt. Mwigulu amesema wa sasa asilimia 70 ya fedha za mifuko ya maendeleo zitaelekezwa moja kwa moja kwenye mifuko husika ili uweze kutekeleza majukumu yake ya kimsingi.

Amesema uamuzi huo utaongeza kasi na uhakika wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupanua wigo wa huduma za jamii na kuongeza fursa za uzalishaji. Uamuzi huo unatokana na ushauri uliotolewa na Wabunge kwa Serikali wakiitaka ichukue hatua za haraka kuwezesha sekta mbalimbali ikiwemo maji, barabara na umeme zinapata fedha kwa wakati.

“Nitumie fursa hii kuwakumbusha watendaji wa taasisi ambazo zitapelekewa fedha hizo, wahakikishe wanakamilisha miradi iliyokusudiwa, tena kwa kuzingatia thamani ya fedha na miradi iwe na uimara. Wakumbuke kuwa dhamira na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa Watanzania,” amesisitiza.

Akitoa mwelekeo wa bajeti na vipaumbele vya sekta kwa mwaka 2026/2027, Dkt. Mwigulu amesema vipaumbele vya kila wizara za kisekta vimezingatia maslahi mapana ya Taifa na kwamba bajeti ijayo itaendelea kuimarisha uwekezaji katika sekta za uzalishaji, miundombinu na huduma za jamii. 

“Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha mifumo ya mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje. Mkakati mmojawapo ni kupunguza utegemezi kutoka nje,” amesisitiza.

Amesema bajeti hiyo inaenda kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ambayo inaajiri zaidi vijana na wanawake. Kupitia utaratibu mpya wa utoaji mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, Waziri Mkuu amezielekeza taasisi za fedha na waratibu wa mikopo hiyo kuondoa masharti magumu yanayokwamisha wajasiriamali kunufaika na mikopo hiyo. 

“Mfano ni ulazima wa wahitaji kwa upande wa watu wenye ulemavu kutakiwa kuunda vikundi na ulazima wa wahitaji kuwasilisha dhamana kubwa kama vile hati za nyumba ambavyo kwa asili ya biashara zao, hawawezi kuwa navyo,” amesisitiza.