Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za intaneti ya kasi ifikapo mwaka 2030, hatua inayolenga kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya teknolojia.
Akizungumza Juni 25 , 2026 baada ya kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ya Usimamizi wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Intaneti ya Kasi kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mtumba jijini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha mtandao wa kasi unapatikana nchini kote bila kuacha maeneo ya pembezoni.
Amesema kuwa kikao hicho ni hatua muhimu katika kuweka mikakati itakayosaidia kufanikisha upatikanaji mpana wa huduma za intaneti ya kasi, huku akibainisha kuwa maendeleo ya sekta hiyo yatasaidia kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi sasa asilimia 94 ya Watanzania tayari wamefikiwa na huduma za intaneti ya kasi, huku asilimia 35 wakipata huduma za teknolojia ya 5G.
Aidha, amebainisha kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na kuongeza kuwa huduma za intaneti ya kasi zitachochea maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, biashara na huduma za serikali mtandaoni.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Moses Mwasaga ameongeza kuwa kamati hiyo ina jukumu la kuhakikisha matumizi ya intaneti ya kasi yanachochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali kupitia sera, miongozo na mikakati rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Amebainisha kuwa Tanzania inapaswa kuendelea kuimarisha ushindani wake katika masoko ya kikanda na kimataifa, ili kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuhakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na maendeleo ya TEHAMA.
Aidha,Serikali imeendelea kusisitiza kuwa kupitia Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Intaneti ya Kasi, ina lengo la kuhakikisha huduma za mtandao zinapatikana kwa usawa mijini na vijijini, ili kujenga jamii jumuishi ya kidijitali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
