Na Happy Lazaro, Arusha 
Wanawake katika Afrika Mashariki wametakiwa kuchangamkia fursa za teknolojia, elimu ya STEM na mitandao ya ufadhili ili kuepuka kuachwa nyuma katika mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea kwa kasi duniani. 
Wito huo umetolewa jijini Arusha leo na  Rebecca Alitwala Kadaga  Mwanasheria wa Uganda na  Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mjadala wa wanawake wa kizazi na kizazi uliofanyika Arusha, ukisisitiza umuhimu wa kuanzisha majukwaa rafiki yatakayowaunganisha wawekezaji, wabunifu, wataalamu na wasichana wanaosomea masomo ya sayansi na teknolojia.
Akichangia mjadala huo, mzungumzaji alisema kuna umuhimu wa kuwa na mifumo inayowawezesha wanawake kupata ushauri, ufadhili na mafunzo ya kitaalamu kupitia programu za kikanda, kitaifa na zile maalumu kwa sekta husika, ikiwemo afya ya kidijitali na ubunifu wa kiteknolojia.
 Alisema majukwaa hayo yanaweza kusaidia kutumia kwa ufanisi rasilimali zilizopo, kupanua mtandao wa kitaalamu na kuwawezesha wanawake kuchangamkia fursa zinazojitokeza katika sekta ya TEHAMA barani Afrika.
Aidha, alitaja umuhimu wa taasisi na mitandao ya kiteknolojia ya ndani na ya bara la Afrika inayojihusisha na kukuza uongozi, ushauri elekezi, upatikanaji wa mitaji na utetezi wa masuala ya TEHAMA. Kwa mujibu wake, taasisi hizo zina nafasi kubwa ya kuwajengea wanawake ujasiri wa kuingia katika taaluma za teknolojia, kuongeza uwakilishi wao katika nafasi za uongozi wa kidijitali, pamoja na kusukuma mbele ajenda ya usawa katika ajira za sekta hiyo.
Katika kuonesha ukubwa wa changamoto iliyopo, alirejea takwimu za utafiti alioufanya katika chuo kikuu kimoja jijini Nairobi, zilizoonesha pengo kubwa la kijinsia katika kozi za sayansi ya kompyuta. 
Alisema mwaka 2020 katika ngazi ya stashahada ya sayansi ya kompyuta kulikuwa na wavulana 24 na wasichana 10, huku mwaka 2021 kukiwa na wavulana saba na wasichana wawili. 
Katika shahada ya kwanza ya sayansi ya kompyuta, mwaka 2020 kulikuwa na wavulana 52 dhidi ya wasichana 11, mwaka 2021 wavulana 43 na wasichana 16, na mwaka 2022 wavulana 50 dhidi ya wasichana tisa. Kwa upande wa shahada ya uzamili ya masomo ya kompyuta, takwimu hizo zilionesha idadi ya wasichana ikiwa ndogo sana au kutokuwepo kabisa katika baadhi ya miaka.
Kutokana na hali hiyo, alisisitiza kuwa mjadala kuhusu STEM haupaswi kubaki katika ngazi ya sera pekee, bali lazima uanze mapema katika mfumo wa elimu ili kuwajengea wasichana msingi imara wa kuingia katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Alitoa rai kwa wadau wa maendeleo, taasisi za kifedha na washirika wa sekta binafsi kuanzisha na kuongeza ufadhili wa masomo, hasa kwa wasichana wanaotaka kusomea masomo ya sayansi na teknolojia, ili kuwasaidia kushindana katika dunia ya sasa ya kidijitali.
Sambamba na hilo, alieleza kuwa mafanikio ya wanawake katika anga ya mtandao hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira salama ya kidijitali.
 Alisema unyanyasaji wa mtandaoni ni miongoni mwa sababu zinazowakatisha tamaa wanawake wengi kutumia au kujihusisha kikamilifu na majukwaa ya kidijitali. 
Kutokana na changamoto hiyo, alitaka kuwepo kwa mapitio ya sheria na sera za kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni na unyanyasaji wa kidijitali, ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanakuwa salama wanapotumia intaneti kwa ajili ya kujifunza, kufanya kazi na kujenga mitandao ya kitaaluma.
Akihitimisha, mzungumzaji aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutokubali wanawake wa Afrika Mashariki kubaki nyuma wakati dunia ikisonga mbele kwa kasi katika mapinduzi ya teknolojia. 
Alisema wanaume tayari wanasonga mbele katika sekta hiyo, hivyo wanawake hawana budi kutumia fursa zilizopo, kutafuta ufadhili, kuwekeza katika elimu ya sayansi na kuendelea kusukuma mabadiliko ya sera yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali. 
Aliahidi ushirikiano na kuunga mkono mapendekezo yatakayotokana na mjadala huo kwa manufaa ya wanawake wa sasa na vizazi.