Na OWM – TAMISEMI, Lushoto

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wananchi wa Wilaya ya Lushoto Gari la kuhudumia wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo, ambalo limekabidhiwa kwa wananchi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Wazo Mwang’onda.

Prof. Shemdoe ametoa shukrani hizo kwa Mhe. Rais kwa niaba ya wananchi wa Lushoto, leo Juni 26, 2026 wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani humo ukitokea wilaya ya Bumbuli, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kizala Lushoto.

“Tuna mshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia gari la kuhudumia wagonjwa katika hospitali ya wilaya, kwani gari lililokuwa likitumika katika hospitali hiyo lilipelekwa kata ya Mlola ambayo ni miongoni mwa kata 33 za wilaya ya Lushoto, ambayo ina vituo vya afya nane (8) na kati ya hivyo ni vinne tu ndio vina magari ya kuhudumia wagonjwa,” ameeleza Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Wazo Mwang’onda, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendelea kusogeza huduma za afya msingi karibu na wananchi kupitia ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, ikiwa ni pamoja na kupeleka magari ya kuhudumia wagonjwa katika vituo mbalimbali vya afya.

“Leo hapa tumeshuhudia gari jipya ambalo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelileta Lushoto, nami nalikabidhi likawahudumie wananchi, na kuongeza kuwa Mwenge wa Uhuru umefurahishwa sana na huduma ambayo Mheshimiwa Rais ameileta kwa wananchi wa Lushoto,” amesema Bw. Mwang’onda.

Mwenge wa Uhuru katika wilaya ya Lushoto umeshakagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa barabara, ujenzi wa hoteli ya kitalii, ukarabati wa matenki ya maji, umaliziaji wa madarasa, mradi wa vijana pamoja na wa kituo cha afya ambapo kesho asubuhi utakakabidhiwa katika wilaya ya Korogwe.