NA DENIS MLOWE, MAFINGA – IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameziagiza halmashauri kuhakikisha zinachukua hatua za haraka kutekeleza mapendekezo ya wakaguzi wa ndani ya Sekretarieti ya Mkoa (SEA) pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akionya kuwa kupuuza ushauri huo husababisha maagizo mazito na kuendelea kujirudia kwa hoja za ukaguzi.
Akizungumza katika Baraza Maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Mafinga lililokutana kujadili hoja za ukaguzi wa CAG, Kheri alisema ushauri wa wakaguzi unapaswa kufanyiwa kazi mapema ili kuzuia halmashauri kuingia kwenye wakati mgumu wa kujieleza mbele ya Kamati za Bunge za Usimamizi wa Hesabu za Serikali.
Alieleza kuwa kujirudia kwa hoja zilezile kila mwaka ni dalili ya kutokuzingatia ushauri unaotolewa na mamlaka za ukaguzi, jambo linaloathiri taswira ya halmashauri na kuongeza mzigo wa uwajibikaji kwa viongozi na watendaji.
Mbali na kusisitiza nidhamu katika usimamizi wa fedha za umma
James alizitaka halmashauri kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, huku akisisitiza kuwa mapato hayo yatumike kutekeleza mipango iliyoidhinishwa badala ya matumizi yasiyo katika bajeti ambayo huibua hoja za ukaguzi.
Aidha, alihimiza Halmashauri ya Mji Mafinga kuanza kuwekeza sehemu ya mapato yake katika miradi ya kimkakati na vitega uchumi vitakavyoongeza mapato ya kudumu badala ya kutegemea vyanzo vya sasa pekee.
Alisema Mafinga ina nafasi ya kipekee kutokana na kuwa lango la Nyanda za Juu Kusini, hivyo inaweza kunufaika zaidi kwa kuwekeza katika huduma na biashara zitakazovutia wasafiri na wawekezaji.
Kheri aliwataka viongozi kuhakikisha watumishi wanaobainika kusababisha hasara au hoja za ukaguzi wanachukuliwa hatua za kinidhamu badala ya kushughulikia matokeo ya makosa yao pekee.
Alisema uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja ndiyo msingi wa kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Wakati wa kikao hicho, Menejimenti ya Halmashauri iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa hoja za ukaguzi, ikieleza kuwa hoja kadhaa zimefungwa huku nyingine zikiendelea kutekelezwa. Miongoni mwa hoja zinazoendelea kushughulikiwa ni madai ya zaidi ya shilingi milioni 52.1 yaliyokataliwa na NHIF kutokana na makosa ya kiutendaji na kiufundi.
Katika kuharakisha utekelezaji wa hoja zilizosalia, Mkuu wa Mkoa aliagiza kuundwa kwa kamati maalumu (Task Force) ya kufuatilia hoja zote ambazo bado hazijafungwa.
Alisema kamati hiyo ianze kazi ndani ya wiki mbili na ikamilishe zoezi la kupitia na kufunga hoja ndani ya siku 21, kabla ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Sekretarieti ya Mkoa.
Alisisitiza kuwa changamoto kubwa si kupitisha mapendekezo katika vikao vya Baraza la Madiwani bali ni kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati.
Kheri aliwataka wataalamu wote wanaohusika na hoja za ukaguzi kuwajibika kikamilifu kupitia kamati hiyo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha kila hoja inapata suluhisho la kudumu.
Alisema Halmashauri ya Mji Mafinga imeonyesha uwezo mkubwa katika ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa shughuli za maendeleo, hivyo haipaswi kuruhusu hoja ndogo za ukaguzi kuharibu sifa yake.
Mkuu wa Mkoa aliipongeza Halmashauri ya Mji Mafinga kwa ushirikiano uliopo kati ya madiwani na wataalamu, akisema mafanikio ya halmashauri yanatokana na viongozi kuheshimu ushauri wa kitaalamu na kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na mipango iliyowekwa.




