Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 unatarajiwa kupokelewa Julai 2, 2026 katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo pamoja na shughuli nyingine za maendeleo utazindua rasmi ukumbi wa kisasa wa kimataifa wa sherehe wa Mahina Social Hall, uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 4 hadi kukamilika kwake.Akizungumza, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema Mwenge wa Uhuru utapitia na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa hiyo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 15, ambapo ukumbi huo ukiwa ni sehemu mojawapo ya miradi hiyo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya sekta binafsi.

Amesema miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, miundombinu pamoja na miradi ya vijana, ambayo inalenga kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi wa Moshi.

Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2026, mmiliki wa Mahina Social Hall, Elifuraha Mbwambo, amesema ni heshima kubwa kwa mradi wake kuchaguliwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru, jambo linaloonesha imani ya Serikali katika miradi inayochochea maendeleo ya jamii.

Amesema hatua hiyo ni uthibitisho kuwa uwekezaji binafsi una mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na uchumi, huku akiahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kushirikiana na Serikali katika kuendeleza maendeleo ya Manispaa ya Moshi.