Paris, Ufaransa.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, amekutana na Mheshimiwa Khondker M. Talha, Rais wa Kikao cha 43 cha Mkutano Mkuu wa UNESCO na Balozi wa Bangladesh nchini Ufaransa, kwa lengo la kujitambulisha kufuatia kuanza rasmi kwa majukumu yake katika UNESCO.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu ajenda za UNESCO, hususan namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za elimu, sayansi, utamaduni na mawasiliano, pamoja na nafasi ya Tanzania katika kuendeleza malengo ya shirika hilo.
Balozi Yakubu alitumia fursa hiyo kumwalika Mheshimiwa Talha kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, akieleza kuwa Kiswahili kinaendelea kuwa daraja muhimu la kuimarisha amani, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Talha alimpongeza Balozi Yakubu kwa uteuzi wake na kuahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika kutekeleza majukumu ya UNESCO na kuendeleza ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote. Mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya kirafiki na ya kujenga, yakidhihirisha dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na uongozi wa UNESCO.

