Na Mwandishi Wetu

Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha sanaa na michezo vinakuwa sehemu muhimu ya ajira na maendeleo kwa vijana nchini.

Hayo yamesemwa na Ndugu Emmanuel Shilatu aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya wakati akizindua mashindano ya Kanda ya Kusini ya kusaka vipaji vya sanaa na michezo kwa watoto.

Shilatu amesema Serikali imeweka mkakati wa kuendeleza vipawa na vipaji vya wanafunzi kwa kushirikiana na wadau wa michezo, huku ikiendelea kuboresha mfumo wa elimu ili kuwaandaa vijana kujifunza na kuendeleza amali mbalimbali ikiwemo michezo na sanaa.

“Serikali imeweka vipaumbele vyake katika kuendeleza vipawa na vipaji vya wanafunzi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo. Hivi karibuni Serikali imeboresha mfumo wa elimu kwa ajili ya kuwaandaa vijana kujifunza amali mbalimbali zikiwemo za michezo na vipaji vya sanaa,” amesema Shilatu.

Kwa upande wake, mwandaaji wa mashindano hayo Shirika la Compassion International amesema jukwaa hilo ni fursa kwa watoto na vijana kuonyesha uwezo wao, kukuza vipaji na kujenga mustakabali bora wa maisha.

Amesema mashindano hayo yamelenga kuzingatia ubora, haki, nidhamu na kutoa burudani kwa washiriki na watazamaji.

Naye mzazi wa mmoja wa washiriki, Bi. Prisca Richard, ameonyesha kufurahishwa na mpango huo akisema una nafasi kubwa ya kusaidia kukuza kipaji cha mtoto wake na kumsaidia kutimiza ndoto zake.

Mashindano hayo yameandaliwa na Shirika la Compassion International na yanashirikisha watoto na timu kutoka mikoa ya Kanda ya Kusini ambayo ni Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 26, 2026, ambapo hafla ya kufunga inatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Vijana, Mhe. Joel Nanauka.