Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo
Picha ya Mshtakiwa Amani Elifatio Mlay, aliyekuwa Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, baada ya kutoroka mahakamani siku ya kutolewa hukumu dhidi yake.
……….
Na Happy Lazaro, Arusha 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imethibitisha kumkamata na kumrejesha mkoani hapa mshtakiwa Amani Elifatio Mlay, aliyekuwa Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, baada ya kutoroka mahakamani siku ya kutolewa hukumu dhidi yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumapili, Juni 21, 2026 katika eneo la Mangaka wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara, kufuatia msako uliofanywa baada ya kutoweka akiwa nje kwa dhamana katika shauri la jinai lililokuwa likisikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Arusha.
TAKUKURU ilieleza kuwa Amani alikuwa akikabiliwa na makosa sita, yakiwemo manne ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake, kinyume na sheria za kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na sheria za uhujumu uchumi.
 Makosa hayo yanadaiwa kufanyika wakati akiwa Mratibu wa TASAF, ambapo alitengeneza nyaraka zenye taarifa za uongo zikionesha kuwa mzabuni alikuwa amewasilisha vifaa vya ujenzi kwa ajili ya mradi wa uzio wa Shule ya Msingi Shangarao katika Jiji la Arusha.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, nyaraka hizo zilihusisha vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 64.2.
 Mahakama ilimtia hatiani Januari 16, 2026 katika makosa manne na kumpa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela. 
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alitoroka siku ya kutolewa hukumu, hali iliyosababisha mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwake ili akamatwe na kupelekwa kutumikia adhabu hiyo.
Ngailo amesema baada ya kukamatwa, taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea ili asomewe hukumu hiyo na kuanza rasmi kutumikia kifungo alichopewa. 
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za wahalifu wa vitendo vya rushwa na ubadhirifu, akisisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kuwafuatilia watuhumiwa popote walipo hadi wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria.