Mchekeshaji Emmanuel Mgaya ‘Masanja’ (kulia) akizungumza na wandishi wa habari baada ya kuitikia wito kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi wa kuripoti ofisini na kuhojiwa juu ya mahojiano yake na wananchi juu ya uelewa wa ugonjwa wa Covid-19 (Corona).
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumhoji Masanja juu ya mahojiano yake na wananchi juu ya uelewa wa ugonjwa wa Covid-19 (Corona) aliporipoti leo ofisini kwake jijini Dodoma
……………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Baada ya kupewa masaa 72 awe ameripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi hatimaye leo mchekeshaji Emmanuel Mgaya ‘Masanja’ameitikia wito na kuomba radhi kwa watanzania kutokana video clip yake ya mahojiano na wananchi juu ya Corona.
DC Katambi alimpa Masanja siku tatu kuripoti ofisini kwake ili kuhojiwa na kueleza sababu ya yeye kurikodi kipindi chake akiwahoji wananchi wa Dodoma maana ya Covid19 jambo ambalo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya lililenga kupotosha kwamba wananchi wake hawana uelewa na ugonjwa huo.
Kufuatia wito huo jana Masanja ameripoti na kuhojiwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo aliomba msamaha na kuahidi kutumia nafasi yake kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa Corona.
Akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano, Masanja amempongeza DC Katambi kwa kuwa mwepesi wa kugundua kuwa kulikuwa na shida kwenye kipindi chake alichorusha jambo linaonesha kweli yeye ni kijana na anaenda na spidi ya Rais Magufuli katika kuwatumikia watanzania.
” Niombe radhi kwa kueleweka vibaya lengo la kipindi chetu lilikuwa kuelimisha na siyo kuleta mzaha, namshukuru Mkuu kwa wito wake huu ambao umenisaidia pia kwa namna moja ama nyingine kujua wapi nilipoteleza.
Kama Taifa tunapita kwenye kipindi kigumu kutokana na maambukizi ya ugonjwa huu hivyo tuendelee kuchukua tahadhari zote kama tunavyoelekezwa na wataalamu wetu ili tuzidi kuwa salama,” Amesema Masanja.
Aidh Masanja amemuahidi DC Katambi kuwa atatumia kipawa chake cha kuhubiri pia kuhamasisha watanzania kutumia vitakasa mikono na kufuata masharti yote ambayo yanatolewa na viongozi.
Upande wake DC Katambi amesema hana tatizo binafsi na Masanja wala kituo cha DW ambacho muigizaji huyo anafanyia kazi bali walimuita kwa ajili ya kuwekana sawa.
” Sisi hatuna tatizo binafsi, ukiangalia kipindi kile maudhui yake ni kama kuonesha kwamba watanzania wote na hasa wanadodoma hatuna uelewa na virusi hivi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona.
Kitendo cha kuweka watu wote waliokosea kujua maana ya covid19 ni kuuaminisha umma kwamba Tanzania siyo mahali sahihi kwa kwa kipindi hiki maana wananchi wake hawajui hata maana ya ugonjwa huu, kumbe ni njia zilizotumika ndizo hazikua sawa, hivyo tumemhoji Masanja na baada ya kuelewa na kuomba radhi tumemsamehe,” Amesema Katambi.
Amesema serikali imeendelea kuchukua hatua zote za kuhakikisha zinakabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwataka watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na kumuomba Mungu kama ambavyo Rais Magufuli alielekeza.