Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akikagua orodha ya mahabusu wakati wa ziara ya kutembelea Vituo vya Polisi lengo ikiwa ni kukagua utekelezaji wa maagizo ya serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona ambapo ameagiza Makamanda wa Polisi nchini na Wakuu wa Magereza kuhakikisha watuhumiwa wanaoruhusiwa kupata dhamana kisheria wapewe ili kuepusha misongamano katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto), akizungumza na wananchi waliokusanyika nje ya Kituo cha Polisi Kati kilichopo wilaya ya Dodoma Mjini ambapo ameagiza wananchi hao kuhudumiwa haraka ili kuepusha misongamano ikiwa ni kutekeleza maagizo ya serikali ya kutokuwepo kwa mikusanyiko ili kupambana na ugonjwa wa Corona.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
……………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Serikali imewaagiza Makamanda wa Polisi na Wakuu wa Magereza mikoa yote nchini kuhakikisha inawapa dhamana mahabusu wote wanaokidhi vigezo vya dhamana na kuharakisha upelekwaji haraka wa kesi kwa watuhumiwa waliopo katika magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuepusha na kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona(Covid 19) usiweze kuingia katika mahabusu za polisi na magereza.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Vituo mbalimbali vya Polisi mkoani Dodoma ambapo alibaini kuwepo msongamano wa mahabusu katika vituo vya polisi huku akifanikiwa kuzungumza na baadhi ya mahabusu ambao ilionekana kesi zao zinadhaminika huku wengine wakiruhusiwa katika ziara hiyo.
“Maagizo ya Serikali na wataalamu wa afya ni kuepusha misongamano sasa nimetembelea kituo hiki cha kati nimekuta mahabusu wengine wamekaa siku kumi na nne,na wengine wanaingia wakiwa wametoka nje huko hali iliyopelekea msongamano mkubwa katika kituo hiki, na kuna mahabusu mmoja nimekuta wamemuweka siku tatu hapa kosa lake wamemkamata tu anapita nje ya bunge hii sio sawa huku hana kosa lolote.
“Sasa natoa maagizo kwa Makamanda wa Polisi nchi nzima katika kukabiliana na ugonjwa wa corona wahakikishe mahabusu wote ambao kesi zao zinadhaminika watolewe, agizo hili pia liende kwa wakuu wa magereza yote nchini kuhakikisha watuhumiwa wote kesi zao zinaharakishwa kupelekwa mahakamani hii yote ikiwa ni mkakati wa kupambana na gonjwa la Corona sasa watu wamerundikwa tu hakuna kinachoendelea hii si sawa” alisema Masauni
Pia alipata fursa ya kuzungumza na wananchi waliokusanyika nje ya vituo vya polisi wakija kuwaona ndugu zao huku akisisitiza washughulikiwe haraka kwani wamekusanyana wengi huku serikali ikiwa imepiga marufuku mkusanyiko wa watu na wataalamu wakishauri umbali kati ya mtu na mtu uwe mita moja.
“Wananchi wamekuja kuona ndugu zao waliopo mahabusu tunajua ni haki yao pamoja na kuwaletea chakula lakini muwahudumie haraka waondoke hii mikusanyiko ishakatazwa ni hatari sana” alisema Masauni.