Na. Sixmund Begashe, MNRT.
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeibuka Mshindi wa Kwanza wa Tuzo ya taasisi iliyofanya vizuri katika Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo iliyokabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Bernard Marcelline, ameitaja tuzo hiyo kama alama muhimu ya kazi kubwa iliyofanya na viongozi wa Wizara hiyo na taasisi zake pamoja na watumishi wake wote.
Bw. Marcelline amewapongeza kwa kazi kubwa na yakutukuka watumishi wote waliohusika katika maandalizi ya maonesho hayo na walioshiriki kuwahudumia vyema wananchi katika Maadhimisho hayo yaliyo hitimishwa leo Juni 23, 2026 Jijini Dodoma.
Aidha baada ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi kutangaza ushindi huo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wananchi walifurahi kwa shangwe huku wakisikika wakisema kuwa, Wizara hiyo imestahili tuzo hiyo kutokana na mvuto wa banda lao, idadi kubwa ya ya taasisi zilizoshiriki na huduma nzuri walizotoa ikiwemo ya tiba ya nyuki iliyotolewa kwa mamia ya wananchi.

