Na Meleka Kulwa-Fullshangwe, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa Tanzania inaendelea kujivunia uwepo wa akiba kubwa ya gesi asilia ambayo imekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya nishati na uchumi wa taifa.
Akizungumza Juni 23, 2026 katika Banda la PURA lililopo kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika Jijini Dodoma, Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa PURA imeendelea kusimamia shughuli za utafutaji, uchimbaji na maendeleo ya rasilimali za mafuta na gesi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya nchi.
Amesema kuwa pamoja na Tanzania kuanza utafutaji wa mafuta tangu miaka ya 1950 na kuchimba visima zaidi ya 97, bado nchi haijafanikiwa kupata mafuta ya kibiashara, lakini imefanikiwa kugundua gesi asilia ambayo inaendelea kutumika katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Aidha, amebainisha kuwa matumizi ya gesi asilia yanaendelea kuongezeka duniani kutokana na mabadiliko ya teknolojia na juhudi za kupunguza matumizi ya nishati zinazochafua mazingira, hali inayofanya rasilimali hiyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa Tanzania.
Pia ameongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, jambo linaloongeza mahitaji ya gesi asilia na kutoa fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.
Mhandisi Sangweni amesema kuwa PURA imeendelea kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali za petroli kupitia ajira, utoaji wa huduma na bidhaa pamoja na ushirikishwaji katika miradi mbalimbali chini ya sera ya Local Content.
Aidha, amebainisha kuwa mamlaka hiyo imeanzisha mifumo ya kuwaunganisha wataalamu wa Kitanzania na wawekezaji ili kuongeza ajira na kukuza uwezo wa wazawa kushiriki kikamilifu katika sekta ya mafuta na gesi.
Pia ameongeza kuwa Serikali imeendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Eyasi Wembere pamoja na vitalu vya Lindi na Mtwara vinavyotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumzia changamoto za mabadiliko ya bei ya mafuta duniani, Mhandisi Sangweni amesema kuwa Tanzania imeendelea kuwa katika hali nzuri ya upatikanaji wa mafuta licha ya migogoro ya kimataifa inayotokea katika baadhi ya maeneo ya dunia.
Aidha, amebainisha kuwa nchi za Afrika Mashariki na Kati zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika matumizi na usambazaji wa rasilimali za nishati ili kuhakikisha usalama wa nishati kwa wananchi hata wakati wa changamoto za kimataifa.
Pia ameongeza kuwa Afrika inapaswa kuendelea kutumia rasilimali zake za mafuta, gesi na madini kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake huku ikiendelea kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2026 yamehitimishwa Jijini Dodoma yakihusisha taasisi mbalimbali za umma zilizowasilisha huduma na mafanikio yao kwa wananchi, ambapo MGENI rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka,
