Na: OWM-KAM, Dodoma

Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa ajira za wageni nchini kwa lengo la kuhakikisha ajira hizo zinatolewa kwa kuzingatia sheria na wageni hao wanaoajiriwa wanamiliki vibali halali.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Dkt. Evaline Munisi amesema hayo leo Juni 23, 2026 Bungeni, Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mheshimiwa John John Nchimbi, Mbunge wa Nyasa, ambaye amehoji Je, nini kauli ya Serikali juu ya Wataalam wa kigeni wanaokaa muda mchache na kupatiwa Business Visa ambayo haitambuliwi na Idara ya Kazi.

Dkt. Munisi amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436, vibali vya kazi hutolewa kwa raia wa kigeni wenye mahusiano ya ajira na kampuni au taasisi zinazowaajiri nchini.

Amesema Idara ya Uhamiaji hutoa Pasi ya Biashara (Business Visa) ya muda usiozidi miezi mitatu kwa wageni wanaokuja nchini kutekeleza kazi maalum za muda mfupi bila kuwa na mahusiano ya ajira na kampuni au taasisi wanazozihudumia.

Kwa mujibu wa Dkt. Munisi, amesema miongoni mwa wanaonufaika na pasi hiyo ni wataalam wanaokuja kutoa mafunzo, kufanya shughuli za kitaalam pamoja na kufunga mitambo na mashine katika taasisi mbalimbali nchini.

Aidha, amesema Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano inatambua uwepo wa wageni wanaotekeleza majukumu maalum katika maeneo ya kazi kwa kutumia pasi hizo na kwamba Serikali inaendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji kuhakikisha wageni hao wanazingatia masharti na taratibu za vibali wanavyopewa.

Vilevile, amesema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano alitoa maelekezo kwa maafisa kazi wote nchini kuhakikisha elimu hiyo inawafikia waajiri, mashirika, taasisi na makampuni yote yanayopokea wageni ili kuongeza uelewa wa sheria na wajibu wa kila upande.

Kadhalika, Dkt. Munisi ameonya vitendo vya baadhi ya watu (vishoka) wanaotumia mbinu zisizo halali kuwaleta wageni nchini kwa ajili ya kufanya kazi kinyume cha taratibu, pamoja na kuwawezesha kuendelea kufanya kazi baada ya mikataba yao kuisha kwa kuwatoa nje ya nchi na kurejea tena kwa kutumia pasi nyingine za kuingia nchini. Ameongeza kuwa, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote au taasisi itakayobainika kukiuka sheria na taratibu za ajira za wageni.

“Kwa atakayebainika kwenda kinyume na maelekezo yaliyotolewa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Kila nchi ina sheria zake na taratibu zake, hivyo sheria za Tanzania zilindwe na Watanzania wenyewe. Tutapambana vikali na wanaofanya kinyume na taratibu na sheria za nchi,” amesema Dkt. Munisi.

Kwa upande mwengine, Naibu Waziri Munisi amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na taasisi nyingine husika ili kuhakikisha wageni wanaokuja kufanya kazi nchini wanazingatia masharti ya vibali na nyaraka wanazopewa kwa mujibu wa sheria, hatua ambayo itasaidia kulinda ajira za Watanzania na kuimarisha usimamizi wa soko la ajira nchini.