Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray, leo tarehe 22 Juni, 2026 ametembelea banda la VETA kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Doma.

Naibu Waziri akiwa katika banda la VETA, ametoa pongezi kwa kazi nzuri na kubwa inayofanywa na VETA katika kutoa mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum pamoja na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupitia kampuni Tanzu ya VETA ya Ujuzi.

“Niwapongeze kwa kuongeza ujuzi kwa vijana wetu kwani kupitia ujuzi huo wanaweza 

kujiajiri wenyewe, kwasasa Serikali imewekeza kwa vijana zaidi kujiajiri, sasa ile hoja ya vijana kujiajiri itafanikiwa kama tutafanya uwekezaji mkubwa kwenye vyuo vya VETA,” amesema Qwaray.

Naibu Waziri ameongeza kuwa kijana anapohitimu kidato cha nne au elimu ya juu anaweza Kwenda VETA akapata ujuzi unaomuwezesha kujiari bila kusubiri ajira za Serikali.

Ameongeza kuwa pia ujuzi kwa wananchi una mchango mkubwa katika kufikia malengo ya Dira 2050.

VETA inashiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 Juni, 2026 nakufunguliwa rasmi tarehe 17 Juni, 2026 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwan Kikwete na yanatarajiwa kufungwa tarehe 23 Juni, 2026.