RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua jengo la Tiba Mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC mkoani Kilimanjaro lenye thamani ya Bilioni 17 pamoja na vifaa vyake.
Akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu ujio huo wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa, ziara hiyo ya Rais mkoani hapo ni ya siku moja ambapo anatajiwa kuwasili Julai 24 mwaka huu.
Alisema kuwa, lengo la ziara hiyo ni kuzindua jengo la Tiba ya Mionzi katika hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC ambalo limegharimu Bilioni 17 pamoja na vifaa vyake huku kati ya fedha hizo Serikali ikiwa imechangia Bilioni 5.5.
Babu alisema kuwa, uchangiaji huo wa serikali ni mwendelezo wa serikali kushirikiana na wadau na Taasisi zisizo za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ambapo kila mwezi imekuwa ikitoa fedha Bilioni 1 kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi katika hospitali hiyo.
