▪️Aipongeza Wizara ya Habari Maandalizi AFCON 2027.

Na Adelina Johnbosco – MAELEZO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, ameipongeza Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali na kusema inafanya kazi kubwa ya kuzitangaza shughuli zinazotekelezwa na Serikali pamoja na kuwafikia wananchi.

Prof. Kahyarara amesema hayo Juni 22, 2026, alipotembelea banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na taasisi zake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

“Serikali ina shughuli nyingi zinazofanyika ikiwemo miradi mbalimbali, mipango na malengo kwa ajili ya maendeleo na maslahi ya wananchi, hata ukisema kila siku au kila wiki utoke na kitu kimoja lakini bado inakuwa haitoshi, lakini Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali inajitahidi kwa kufanya kazi kubwa kwani taarifa zinatolewa kuhusu yanayotekelezwa na Serikali kwa wananchi wake” ameongeza Prof. Kahyarara.

Kwa upande mwingine, ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kufikia hatua nzuri katika maandalizi ya AFCON 2027 pia na taifa kwa ujumla kuwa miongoni mwa nchi zilizochaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwaka 2027.

“Hii inaonesha jinsi gani Tanzania imefikia hatua ya juu katika michezo na imeaminika na ina uwezo wa kuhudumia wageni, lakini pia itakuwa fursa ya kuutangaza utamaduni wetu kwa mataifa mengine” – Prof. Kahyarara. 

Aidha, amesema Wizara ya Uchukuzi tayari imejipanga katika sekta zake za usafiri na usafirishaji kwa kuhakikisha inawahudumia wenyeji na wageni kabla, wakati na baadaya ya AFCON 2027.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 23, 2026 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi. Dkt. Moses Kusiluka