Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) zimesaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 20 sawa na takribani Shilingi bilioni 60.7 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo.Akizungumza na waandishi wa habari Juni 22, 2026 Jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba amesema kuwa msaada huo unalenga kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuimarisha huduma za usafi wa mazingira katika maeneo hayo ya miji.

Aidha amebainisha kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji, ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka, pamoja na ununuzi wa magari ya majitaka yatakayosaidia kuboresha huduma za usafi wa mazingira.Pia ameongeza kuwa mradi huo utajumuisha ujenzi wa vyoo katika shule na taasisi mbalimbali za umma ili kuhakikisha mazingira bora ya kiafya kwa wananchi hususan wanafunzi na watumishi wa umma.

Amesema kuwa Serikali ya Tanzania, inaendelea kuthamini ushirikiano wa muda mrefu na Serikali ya ujerumani ambao umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika sekta za maji, afya, mazingira na usimamizi wa fedha za umma.

Ameongeza kuwa mradi huo pia unalingana na mipango ya maendeleo ya taifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Dira mpya ya 2050 pamoja na mipango ya maendeleo ya miaka mitano ya taifa.

Aidha amebainisha kuwa katika majadiliano ya Serikali hizo mbili yaliyofanyika Machi 20, 2024 jijini Dar es Salaam, Serikali ya Ujerumani iliahidi kutoa msaada wa Euro milioni 70 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.

Dkt. Mwamba amesema kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Ujerumani ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania na KFW zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya maji nchini.Naye Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW), Bi. Vanessa Eidt amesema kuwa ushirikiano huo utaendelea kuleta matokeo chanya kwa wananchi kupitia uwekezaji katika miradi ya kijamii na miundombinu muhimu.