Na John Bukuku, Dar es Salaam

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar pamoja na Yas Fiber Tanzania, Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma bora za mawasiliano na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Alisema tayari utekelezaji wa mradi huo umeanza kabla hata ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo, jambo linalodhihirisha dhamira ya dhati ya pande zote mbili katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa haraka.

Waziri Soraga alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuweka mazingira bora ya kuimarisha miundombinu ya kidijitali kwa kuwa teknolojia imekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika dunia ya sasa.

“Miundombinu ya kidijitali ni msingi wa uchumi wa kisasa. Ushirikiano huu utaharakisha mageuzi ya kidijitali na kusaidia kuiweka Zanzibar katika nafasi ya kuwa miongoni mwa vinara wa uchumi wa kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema.

Kupitia makubaliano hayo, Yas Fiber Tanzania itawekeza takriban shilingi bilioni 300 kwa kipindi cha miaka 20 kwa ajili ya kupanua huduma za intaneti yenye kasi visiwani Zanzibar kupitia ujenzi na upanuzi wa mtandao wa mkonga wa mawasiliano (Fiber).

Uwekezaji huo unatarajiwa kuiwezesha huduma ya mkonga wa mawasiliano kuwafikia takriban kaya 100,000 katika visiwa vya Unguja na Pemba ndani ya miaka mitatu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi.

Mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti zenye kasi, uhakika na nafuu kwa wananchi, biashara, taasisi za elimu, vituo vya afya pamoja na taasisi za Serikali, huku ukiunga mkono azma ya Zanzibar kuwa kitovu cha ubunifu, uwekezaji na huduma za kidijitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, alisema ushirikiano huo utaongeza kasi ya upanuzi wa huduma ya mkonga wa mawasiliano na kusaidia wananchi wengi zaidi kupata huduma bora za mawasiliano.

“Ushirikiano huu utawezesha wananchi na taasisi nyingi zaidi kupata huduma ya intaneti yenye kasi na kuchangia ujenzi wa miundombinu ya kidijitali inayohitajika kwa maendeleo ya Zanzibar ya sasa na ya baadaye,” alisema Mhandisi Suleiman.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas Fiber, Maxime Woimant, alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono ajenda ya mageuzi ya kidijitali nchini na kuchangia maendeleo jumuishi kupitia mawasiliano ya kisasa.

Alisema uwekezaji huo ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya kidijitali kufanyika Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni, ambao utawezesha biashara kukua, wanafunzi kupata fursa za kujifunza na jamii kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Mradi huo utatekelezwa chini ya mfumo wa Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ZICTIA itatoa ushirikiano katika masuala ya uratibu wa kikanuni, upatikanaji wa maeneo ya utekelezaji na usimamizi wa mradi.

Mbali na uwekezaji wa miundombinu, ushirikiano huo pia unatarajiwa kuchangia maendeleo ya ujuzi wa kidijitali, uhamishaji wa maarifa na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani ili kuwawezesha kushiriki katika uchumi unaoendeshwa na teknolojia.