Balozi Mahamoud Thabit Kombo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
…………….
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Katika dunia ya sasa ya mawasiliano, mwandishi wa habari si mtu anayebeba kalamu, kamera au kinasa sauti pekee, bali ni mtaalamu anayebeba wajibu wa kuwakilisha taaluma yake, chombo cha habari anachokifanyia kazi na wakati mwingine taswira ya nchi yake.
Kutokana na nafasi hiyo, kuna umuhimu mkubwa wa kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa somo la itifaki kwa waandishi wa habari katika vyuo vinavyofundisha taaluma hiyo au kuanzishwa kwa kozi maalum itakayowajengea uwezo wa kuelewa namna ya kuenenda katika mazingira mbalimbali ya kazi.
Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu baadhi ya waandishi wa habari kutokuzingatia mambo muhimu ya mwenendo na taratibu wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa wanapofanya kazi kwenye mikutano ya viongozi, ziara rasmi, hafla za kitaifa na mikutano ya kimataifa.
Hali hiyo imekuwa ikionekana katika maeneo mbalimbali ambapo wakati mwingine baadhi ya waandishi huonekana kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kujiweka katika mazingira yanayohitaji utaratibu maalum.
Jambo hili halimaanishi kwamba waandishi wote hawafuati taratibu, kwa sababu wapo wengi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa, lakini changamoto hizo zinaonesha umuhimu wa kuongeza elimu ya itifaki ndani ya taaluma ya habari ili kuhakikisha kila mwandishi anakuwa tayari kufanya kazi katika mazingira yoyote.
Itifaki mara nyingi imekuwa ikihusishwa na viongozi, wageni wa kimataifa au maafisa wa serikali, lakini ukweli ni kwamba mwandishi wa habari naye anakutana na mazingira hayo na anapaswa kuwa na uelewa wa msingi kuhusu taratibu zinazotawala maeneo hayo. Mwandishi anapokuwa katika msafara wa kiongozi, mkutano wa kimataifa au hafla rasmi, anahitaji kufahamu namna ya kuwasiliana, namna ya kuvaa kulingana na mazingira, namna ya kuomba mahojiano, muda sahihi wa kuuliza maswali na mipaka ya eneo analopaswa kufanyia kazi.
Balozi Mindi Kasiga Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Elimu ya itifaki inaweza kusaidia kujenga heshima zaidi kwa taaluma ya habari kwa sababu mwandishi anapojua namna ya kuenenda anakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake bila kuathiri utaratibu wa tukio.
Katika mikutano mikubwa ya viongozi, kila jambo huwa na mpangilio wake kuanzia namna ya kuingia ukumbini, sehemu za kukaa, muda wa kuchukua taarifa, hadi namna ya kushirikiana na waandaaji wa tukio.
Kwa uzoefu wangu binafsi kama mwandishi wa habari, nimepata nafasi ya kufanya kazi na kuripoti matukio mbalimbali ya viongozi wakuu wa nchi kuanzia kipindi cha Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, Awamu ya Nne ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete, Awamu ya Tano ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na sasa katika Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika kipindi hicho nimekutana na mazingira mengi yanayohitaji uelewa wa masuala ya kiitifaki na kwa kiasi fulani nimejifunza kutokana na uzoefu wa kazi, maelekezo ya waandaaji wa matukio na uzoefu wa muda mrefu katika tasnia ya habari.
Hata hivyo, ninaamini kabisa kwamba kama ningepata mafunzo rasmi ya itifaki hata kwa muda mfupi, ningekuwa na uelewa mpana zaidi wa namna bora ya kufanya kazi katika mazingira hayo.
Hii ndiyo sababu ninaona umuhimu mkubwa wa waandishi wa habari kupatiwa semina na mafunzo maalum yatakayowaongezea uelewa wa masuala ya itifaki.
Mwandishi anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kuandika habari, kufanya mahojiano na kuchanganua matukio, lakini kuongeza maarifa ya itifaki kutamfanya awe mtaalamu aliyekamilika zaidi, anayejua namna ya kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kujiamini katika mazingira mbalimbali.
Mwandishi wa habari anapaswa pia kuelewa kuwa mavazi yake ni sehemu ya taswira ya taaluma yake. Suala hili si kwamba mwandishi anatakiwa kuvaa kwa gharama kubwa, bali ni kuzingatia mazingira ya kazi anayokwenda kufanya.
Kuna tofauti kati ya kuripoti tukio la kawaida la kijamii na kwenda kwenye mkutano wa viongozi wakuu wa nchi au tukio la kidiplomasia. Uelewa wa itifaki unaweza kumsaidia mwandishi kufanya uchaguzi sahihi wa mavazi na mwonekano unaoendana na mazingira husika.
Pamoja na hayo, itifaki inaweza kumsaidia mwandishi kuboresha namna ya kuwasiliana na viongozi na watu mbalimbali anaokutana nao katika kazi zake. Uhuru wa mwandishi kuuliza maswali hauondolewi na itifaki, bali unajengwa zaidi kwa kuwa mwandishi anafahamu namna bora ya kufikisha ujumbe wake bila kuvunja taratibu za eneo husika.
Katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kushiriki na kuandaa mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, waandishi wa habari wanazidi kupata nafasi ya kukutana na viongozi wa mataifa mbalimbali, mabalozi, mashirika ya kimataifa na watu wenye nafasi kubwa katika jamii.
Hivyo, maandalizi ya mwandishi hayawezi kubaki kwenye uwezo wa kuandika habari pekee, bali yanahitaji pia uelewa wa namna ya kufanya kazi katika mazingira yenye taratibu maalum.
Ni muhimu kuelewa kwamba kufundishwa itifaki hakumaanishi kumzuia mwandishi kuwa huru katika kazi yake. Badala yake, ni kumpa uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kama ambavyo taaluma nyingine zina taratibu zake, ndivyo ambavyo uandishi wa habari unavyohitaji mwandishi kuelewa namna ya kujiendesha katika mazingira tofauti.
Vyuo vinavyofundisha uandishi wa habari vinaweza kuangalia uwezekano wa kuwa na somo maalum la itifaki, mwenendo na mawasiliano ya kitaaluma kwa waandishi wa habari. Somo hilo linaweza kuwasaidia wanafunzi kuelewa namna ya kufanya kazi kwenye hafla rasmi, mikutano ya kimataifa, uhusiano na viongozi, maadili ya mwandishi katika mazingira rasmi na namna ya kujiwakilisha mbele ya jamii.

Kwa waandishi ambao tayari wapo kazini, taasisi za habari, vyama vya waandishi wa habari na wadau wengine wanaweza kuanzisha mafunzo mafupi ya mara kwa mara kuhusu masuala haya ili kuwajengea uwezo zaidi.
Taaluma ya habari inaendelea kubadilika na majukumu ya mwandishi yanaongezeka kila siku. Mwandishi wa leo si mtoa taarifa pekee, bali ni mtaalamu anayekutana na watu wa ngazi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa hiyo, kuwa na elimu ya itifaki kutasaidia kujenga waandishi wenye weledi mpana, wanaojua haki zao, wajibu wao na namna ya kuiwakilisha taaluma yao kwa heshima.
Ubora wa mwandishi haupimwi kwa habari anayoandika pekee, bali pia namna anavyowasilisha taaluma yake mbele ya jamii.
Uvaaji wake, namna anavyokaa mbele za watu, namna anavyokula na hata namna anavyowasiliana ni sehemu ya taswira yake kitaaluma. Ndiyo maana elimu ya itifaki inapaswa kupewa nafasi katika malezi ya waandishi wa habari wa sasa na wa kizazi kijacho kinachokabiliwa na changamoto nyingi za utandawazi katika dunia ya leo.
