Mashamba darasa
NA DENIS MLOWE IRINGA
JUA la asubuhi linapoangaza katika kijiji cha Ikuka, Kata ya Uhambingeto, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Fausta Kikombe anasimama katikati ya shamba lake la alizeti akitazama mimea iliyostawi vizuri.
Kwa miaka miwili aliyojihusisha na kilimo cha alizeti, matokeo aliyokuwa akiyapata hayakumtia moyo licha ya kutumia muda na nguvu nyingi shambani, mavuno yalikuwa madogo na kipato hakikutosha kukidhi mahitaji ya familia.
“Nilikuwa nalima takribani heka moja na nusu na kuvuna gunia mbili tu. Tulikuwa tunalima kwa mazoea, bila kufuata kanuni bora za kilimo hivyo kipato kilikuwa kidogo sana na wakati mwingine tulilazimika kuuza mazao kwa bei yoyote ili kupata fedha za matumizi ya nyumbani,” anasema Fausta.
Leo, matumaini yake yamebadilika.
Kupitia mafunzo ya kilimo bora yanayotolewa na Ruaha Milling Company Ltd kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, anaamini heka moja inaweza kuzalisha kati ya gunia 12 hadi 15 za alizeti.
“Kwa elimu tuliyoipata nimeona tofauti kubwa. Sasa ninaamini alizeti inaweza kuwa biashara ya kweli na si zao la ziada kama tulivyokuwa tunafikiri zamani,” anasema.
Fausta ni mmoja wa mamia ya wakulima wa Mkoa wa Iringa wanaonufaika na juhudi za Ruaha Milling Company Ltd za kuimarisha uzalishaji wa mazao na kuboresha maisha ya wakulima kupitia elimu, masoko na uwezeshaji wa kilimo cha kisasa.
SAFARI YA KAMPUNI INAYOJENGA NGUVU YA MKULIMA
Ruaha Milling Company Ltd ni kampuni inayojishughulisha na uchakataji wa mazao ya kilimo na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao hayo.
Kwa mujibu wa Meneja wa Masoko wa kampuni hiyo, Yasinta Athanasi Kipeto, kampuni ilianza shughuli zake mwaka 1995 kabla ya kusajiliwa rasmi kama kampuni mwaka 2015.
Leo kampuni imejikita katika mazao makuu matatu; mpunga, mahindi na alizeti mazao hayo hununuliwa kutoka kwa wakulima wa Iringa pamoja na mikoa jirani ya Njombe, Ruvuma na Mbeya.
“Tunategemea mkulima kwa kila hatua ya biashara yetu kwani mafanikio ya kampuni hayawezi kutenganishwa na mafanikio ya mkulima na ndiyo maana tunawekeza sana kwenye elimu na uwezeshaji wa wakulima,” anasema Yasinta.
Anasema moja ya mambo ambayo kampuni imekuwa ikiyasisitiza ni matumizi ya mizani katika ununuzi wa mazao ili kuhakikisha mkulima anapata thamani halisi ya kile alichokizalisha.
“Mkulima anapouza kwa mizani anajua amezalisha kiasi gani na amepata kiasi gani hii inamsaidia kufanya kilimo kwa mtazamo wa biashara badala ya mazoea,” anasema.
Yasinta anasema kuwa kampuni imekuwa ikifanya kazi ya kubadilisha fikra za wakulima ili waone kilimo kama biashara yenye faida na si shughuli ya kujikimu pekee.
KILIMO KAMA BIASHARA, SI UTAMADUNI
Katika maeneo mengi ya vijijini, kilimo bado kinafanywa kwa mazoea na bila kuzingatia hesabu za biashara hali hiyo ndiyo ambayo Ruaha Milling imeamua kuibadilisha mbali na kutoa elimu ya kilimo bora, kampuni imekuwa ikiwaunganisha wakulima na taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo ya kuongeza uzalishaji.
“Tuna wakulima wenye ardhi kubwa lakini wanalima sehemu ndogo kwa sababu ya ukosefu wa mitaji tunapowaunganisha na taasisi za fedha na kuwahakikishia soko, wanapata uwezo wa kuongeza uzalishaji na kipato,” anasema Yasinta.
Anaongeza kuwa uwekezaji kwa mkulima ni uwekezaji kwa biashara endelevu ya kampuni, kwa kuwa ubora na wingi wa malighafi hutegemea uwezo wa mkulima kuzalisha.
TATIZO LILILOWARUDISHA SHAMBANI
Kwa miaka ya karibuni, uzalishaji wa alizeti katika baadhi ya maeneo umekuwa ukipungua huku ubora wa mazao ukiwa wa kiwango kisichokidhi mahitaji ya viwanda.
Afisa Shamba Msaidizi wa Ruaha Milling Company Ltd, Benjamini Laurence Mbilo, anasema changamoto hiyo ndiyo iliyoifanya kampuni kuamua kurudi mashambani na kufanya kazi moja kwa moja na wakulima.
“Alizeti nyingi tulizokuwa tunanunua zilikuwa na ubora wa chini hii ni kwa kuwa zilikuwa na mapepe mengi na mafuta kidogo ,tulikuwa tunapata mashudu mengi kuliko mafuta. Hapo ndipo tukagundua kuwa suluhisho ni kuwafikia wakulima na kuwapa elimu ya kilimo bora,” anasema.
Kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa katika vijiji mbalimbali, wakulima wamekuwa wakipata mafunzo ya maandalizi ya mashamba, matumizi ya mbegu bora, upandaji kwa nafasi sahihi, matumizi ya mbolea, uvunaji na uhifadhi wa mazao.
Mbilo anasema kampuni pia imekuwa ikitoa pembejeo kwa mfumo wa mikopo bila riba, huku wakulima wakirejesha thamani ya pembejeo hizo kupitia mazao wanayouza baada ya mavuno.
USHIRIKIANO UNAOMWEZESHA MKULIMA
Katika utekelezaji wa programu hizo, Ruaha Milling imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo CIAT kupitia mradi wao wa “Growing Together” au “Tukue kwa Pamoja”.
Bibi Shamba wa CIAT, Inot Ibrahim Songoyani, anasema lengo la mradi huo ni kuhakikisha mkulima anazalisha kwa tija huku akikabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunahamasisha wakulima kupima afya ya udongo, kutumia mbolea za asili kama samadi na kutumia mbegu bora zinazoweza kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema.
Anasema kupitia mashamba darasa, wakulima wameweza kuona kwa macho tofauti kati ya mbegu bora za kisasa na mbegu za kawaida walizokuwa wakitumia hapo awali.
“Tunaamini mkulima akipata elimu sahihi, pembejeo sahihi na soko la uhakika, basi kipato chake kitaongezeka kwa kiwango kikubwa,” anasema.
MAHITAJI MAKUBWA YA SOKO
Licha ya mafanikio yaliyopo, mahitaji ya malighafi kwa viwanda vya Ruaha Milling bado ni makubwa kuliko kiwango kinachopatikana kwa sasa.
Yasinta anasema kampuni ina viwanda vitatu vikuu vya kuchakata mpunga, mahindi na alizeti, lakini upatikanaji wa malighafi bado ni changamoto.
“Tunahitaji zaidi ya gunia 15,000 za alizeti kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya soko, lakini bado hatujafikia kiwango hicho kutokana na uzalishaji mdogo mashambani,” anasema.
Anabainisha kuwa kiwanda cha mafuta kina uwezo wa kuchakata kati ya gunia 50 hadi 60 za alizeti kwa siku, huku kila gunia la kilo 70 likitoa wastani wa lita 20 za mafuta.
“Ndiyo maana tunaendelea kurudi mashambani. Tunataka mkulima azalishe zaidi, apate kipato kizuri na sisi tupate malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vyetu,” anasema.
VIONGOZI WA KIJIJI WAONA MATOKEO
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuka, Salum Maginga, anasema kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
Anasema ujio wa Ruaha Milling umeleta mwamko mpya kwa wakulima kwa kuwapatia elimu ya kilimo bora pamoja na kuwafundisha namna ya kutunza ardhi kwa ajili ya uzalishaji endelevu.
“Wananchi wetu wanategemea kilimo kwa maisha yao ya kila siku. Kupitia elimu hii wameanza kuona kilimo kwa mtazamo mpya na tunaamini uzalishaji utaongezeka zaidi,” anasema.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Ikuka, Zakia Mpogole, anasema wananchi wengi wa kijiji hicho hutegemea kilimo kwa karibu kila jambo la maisha yao.
“Kilimo ndicho msingi wa maisha ya wananchi wetu kiimekuwa kikibadilisha maisha yao na kinaendelea kufanya hivyo. Kupitia elimu inayotolewa sasa tunaamini wakulima wataongeza uzalishaji na kipato chao,” anasema.
MBEGU YA MATUMAINI
Kwa Fausta na wakulima wengine wa Ikuka, elimu waliyoipata imekuwa zaidi ya mafunzo ya kilimo; imekuwa mbegu ya matumaini.
Kutoka kuvuna gunia mbili katika heka moja na nusu hadi kuwa na matarajio ya kuvuna gunia 12 hadi 15 kwa heka moja, safari yake inaonyesha namna maarifa yanavyoweza kubadilisha maisha ya mkulima.
“Leo ninaamini ninaweza kufanya kilimo kwa faida. Nikifuata yale yote niliyojifunza, mavuno yataongezeka na maisha yangu yatabadilika,” anasema.
Katika Mkoa wa Iringa, ambako maelfu ya wananchi wanategemea kilimo kwa maisha yao, jitihada za kuunganisha elimu, masoko, teknolojia na ushirikiano wa wadau zinaanza kuzaa matunda.
Na kwa Ruaha Milling Company Ltd, safari ya kumwezesha mkulima siyo tu uwekezaji katika biashara, bali ni uwekezaji katika mustakabali wa uchumi wa vijijini na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

