📍DODOMA

Tume ya Madini imeendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa leseni za madini nchini kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya leseni hizo na kuhakikisha shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza katika Banda la Tume ya Madini kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park mkoani Dodoma, Mtakwimu kutoka Kurugenzi ya Leseni ya Tume ya Madini, Azihar Kashakara, amesema ukaguzi huo ni muhimu katika kuhakikisha wamiliki wa leseni wanatimiza masharti na wajibu unaotokana na leseni walizopewa.

Amesema kuwa, pamoja na kufuatilia maendeleo ya leseni, Kurugenzi ya Leseni ina jukumu la kutoa na kusimamia leseni za madini, kutafsiri na kusambaza takwimu za leseni, pamoja na kuwezesha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na umiliki wa leseni hizo.

Kashakara ameeleza kuwa utoaji wa leseni za madini unazingatia masharti na vigezo vilivyowekwa kisheria, hivyo waombaji wanapaswa kuyatimiza ili kuwezesha upatikanaji wa leseni kwa wakati. 

Aidha, ametoa ufafanuzi kuhusu ada na tozo mbalimbali zinazohusiana na leseni za madini, sambamba na kueleza tofauti kati ya umiliki wa ardhi (Surface Rights) na umiliki wa haki za madini (Mineral Rights).

Tume ya Madini ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma chini ya kaulimbiu isemayo, “Kuchochea Uwajibikaji kwa Huduma Endelevu.” 

Kupitia maonesho hayo, wananchi na wadau wa sekta ya madini wanapata fursa ya kuelimishwa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Tume ya Madini pamoja na mchango wake katika usimamizi endelevu wa rasilimali za madini kwa maendeleo ya taifa.