NA MWANDISHI WETU, PANGANI

Kiongozi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda, ameridhishwa na ubora wa miradi ya maendeleo pamoja na thamani ya fedha (value for money) zilizotumika kutekeleza miradi hiyo katika halmashauri ya wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Kiongozi huyo ameyasema hayo Juni 20, 2026, ambapo amesisitiza kuwa miradi yote iliyotekelezwa katika halmashauri hiyo ina ubora, jambo linalothibitisha umakini wa viongozi katika kusimamia miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi na kuchochea maendeleo nchini.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, umeridhishwa na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa Pangani. Hongereni sana viongozi kwa usimamizi mzuri,” amesema Mwang’onda.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema, viongozi ndani ya halmashauri ya Pangani wako makini linapokuja suala lenye maslahi kwa wananchi.

“Tunampongeza Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo, sisi wasaidizi wake tutaendelea kuimarisha usimamizi wa fedha hizo, ili tija iweze kuonekana katika maisha ya wananchi tunaowaongoza,” amesema Aweso.

Katika halmashauri hiyo, miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 imezinduliwa ikiwemo miradi ya barabara, afya, maji, elimu ambayo inatarajiwa kuwanufaisha wananchi.

Halmashauri ya Pangani inatarajiwa kukabidhi mwenge huo kwa halmashauri ya Jiji la Tanga Juni 21. Kwa ujumla, miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 27 inatarajiwa kupitiwa na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru katika halmashauri 11 za mkoa wa Tanga.

Kwa mwaka huu, Mbio za Mwenge wa Uhuru zinachagizwa na kaulimbiu isemayo “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo,” ikiwa ni juhudi za kuhimiza wananchi kushikamana katika ujenzi wa Taifa letu.