NA: MWANDISHI WETU, DODOMA

Watanzania na wapenda maendeleo nchini wameombwa kuishika mkono familia ya Bi.Victoria Mkwizu, aliyejifungua watoto watano, Juni 13, 2026, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ya Jijini Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mary Chatanda, Juni 19, 2026, Jijini Dodoma.

Chatanda amesema watoto ni baraka kutoka kwa Mungu na wanapaswa kupata mahitaji yote muhimu ili waweze kukua wakiwa na afya njema na kufurahia uwepo wao hapa duniani.

“Watoto wale watano wanahitaji mahitaji yote muhimu, tukiiachia familia peke yake watalemewa, hivyo basi, niwaombe Watanzania kwa umoja wetu kama ambavyo tumekuwa tukishikana mkono katika mambo mengi, hebu hata hili tushikamane pia, ili watoto wale waendelee kuwa baraka kwa familia ile badala ya wazazi wao kuwaza matunzo yao kila siku,” amesema Chatanda.

Chatanda ameipongeza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kugharamia gharama zote tangu walipoingia hospitalini hadi watakaporuhusiwa.

“Wenzetu wa Muhimbili wameonyesha moyo wa upendo sana, wamejitoa kugharamia gharama zote za pale hospitalini, sisi wengine hebu tuwaunge mkono wenzetu waliofungua pazia la michango,” amesema.

Katika hatua nyingine, Chatanda amesema amemsikiliza baba mzazi wa watoto hao, Simon Mkwizu, ambaye amekiri kuwa watoto ni baraka lakini pia wanampa mawazo ya namna gani atawalea kutokana na kipato chake kuwa kidogo. 

“Baba mzazi amesema yeye ni dereva bajaji na mkewe ni mama wa nyumbani, anawafurahia watoto wake lakini kwa upande mwingine wanampa stress (msongo wa mawazo) wa namna gani atawalea kutokana na gharama za maisha zilivyo, hebu tuwasaidie wenzetu wale wafurahie baraka ya watoto wao,” amesema.

CHATANDA ATAMANI FAMILIA IPATE NYUMBA MPYA YA KUISHI

Pamoja na mambo mengine, Chatanda amesema anatamani Watanzania washikamame kufanikisha ujenzi wa nyumba mpya ili wazazi wapate utulivu wa kuwalea watoto wao, pamoja na fedha za matunzo yao.

“Natamani wapate nyumba yaani mwenye tofali, mchanga, nondo, mabati, mbao, fedha taslimu kiasi chochote hata kama ni shilingi elfu moja ili tu wawe na makazi yao ya kudumu,” amesema.

Juni 13, 2026, itabaki kuwa siku ya kihistoria kwa Simon na Victoria Mkwizu kwa kupata watoto watano ambao kati yao, watoto wakiume ni watatu na wakike ni wawili. Familia hiyo ni wakazi wa Tabata Jijini Dar es Salaam.