Na WMJJWM – Mwanza. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Maswi, amesema kada ya Maendeleo ya Jamii ndiyo injini ya maendeleo ya Taifa kwa kuwa inajenga uwezo wa wananchi, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kubadilisha changamoto kuwa fursa za maendeleo.

Maswi ameyasema hayo leo 19 Juni, 2026 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) uliofanyika jijini Mwanza. 

Maswi amesisitiza umuhimu wa kuimarisha nafasi ya wataalam wa maendeleo ya jamii katika kufanikisha malengo ya DIRA2050.

“Hakuna taifa linaloweza kuendelea kwa kutegemea miundombinu pekee, bali maendeleo ya kweli hujengwa na watu wenye maarifa, maadili, uzalendo na utayari wa kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao” amesema Maswi.

“Lazima tujiulize Tanzania ya mwaka 2050 itajengwaje na wataalam wa Maendeleo ya Jamii. Ni wakati wa kurudi kwenye misingi ya kada hii na kuimarisha ili mchango wake katika kujenga Taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kushindana, ubunifu, wazalendo na wastahimilivu,” amesema Maswi.

Aidha, Maswi amebainisha kuwa serikali inahitaji wataalam wa Maendeleo ya Jamii wenye uwezo wa kubuni suluhisho kuzalisha mawazo mapya na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji katika mtaji wa watu, kwa lengo la kujenga jamii yenye msingi ya maadili, mshikamano, na uzalendo kwa nchi ya.  

Kwa upande wake, rais wa CODEPATA, Victor Kabuje amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na Wizara katika kuimarisha taaluma ya Maendeleo ya Jamii na kutoa mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Mkutano huo umewakutanisha wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutoka Mikoa na Halmashauri mbalimbali kwa lengo la kujadili mafanikio na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha utendaji katika majukumu yao.