WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wafugaji nchini kuanzisha mashamba ya malisho na kutumia teknolojia za kisasa za ufugaji ili kuongeza tija na kupata suluhisho la kudumu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji inayochangiwa na ongezeko la matumizi ya ardhi.
Akifungua Maonesho ya Tri-Nations Livestock Expo yaliyofanyika Ubena, Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Ijumaa Juni 19, 2026, Dkt. Mwigulu amesema ongezeko la idadi ya watu na matumizi ya ardhi linaifanya nchi kutafuta mbinu endelevu za kuhakikisha shughuli za ufugaji zinaendelea kwa tija bila kuibua migogoro.
“Hata tusingependa kufanya hivyo, hatuna njia nyingine kwa sababu ongezeko la matumizi ya ardhi linalosababishwa na ongezeko la idadi ya watu, huku ardhi ikiwa haiongezeki, linatulazimu kutafuta suluhisho endelevu,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amesema changamoto ya upatikanaji wa malisho inapaswa kwenda sambamba na matumizi ya mbegu bora za mifugo na malisho ili kuwawezesha wafugaji kupata maziwa mengi na nyama nyingi hata kwa kuwa na mifugo michache.
Aidha, Dkt. Mwigulu amewataka wafugaji wa Kitanzania kuyatumia maonesho hayo kama shamba darasa la kujifunza ufugaji bora, wa kisasa na wenye tija ili kuongeza uzalishaji na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wadau wa sekta ya mifugo nchini kuchangamkia fursa za matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi.
“Maonesho hayo yanapaswa kutumika kama darasa la teknolojia na jukwaa muhimu la kununua na kuuza mifugo bora kupitia minada inayoambatana na matukio hayo,” amesema.
Pia, amewataka wazalishaji kuacha utamaduni wa kuandaa bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya maonesho pekee na badala yake waufanye ubora huo kuwa utaratibu wa maisha yao ya kila siku ya kibiashara.
“Ninachokisema ni nini? Tulichokiona katika maonesho haya ndio uwe utaratibu wa maisha. Tusiwe na bidhaa tu kwa ajili ya maonesho; bidhaa za aina hii ndio ziwe bidhaa za kila siku katika maisha yetu,” amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mwigulu amepongeza mchango wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo na mageuzi ya kiuchumi katika sekta ya mifugo, akitaja Mbogo Ranch kuwa mfano wa kuigwa.
Vilevile, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameondoa zaidi ya kodi 300 zilizokuwa zikigusa sekta mbalimbali za uzalishaji kwa lengo la kuendeleza sekta hizo, ikiwemo sekta ya mifugo na sekta nyingine zinazohusiana na uzalishaji.
Kwa Upande wake Waziri wa Mifugo Dkt. Bashiri Kakurwa amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Haasan kwa jitihada zake za kuhakikisha anaikuza na kuiendeleza sekta ya mifugo nchini
Aidha, Amsemea kuwa lengo kuu la maonesho hayo ni kujenga mfungo imara wa biashara wa mifugo na mazao yake kwa kuwakutanisha wafugaji na wafanyabiashara na wadau wote katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo ili kubadlishana uzoefu na kujifunza mbinu za kisasa za ufugaji pamoja na kupanua fursa za masoko nchini
Naye Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, amesema sekta ya mifugo ni muhimu sana katika uchumi wa nchi na inahitaji kusimamiwa vizuri ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa.

