Wakati Afrika ikiadhimisha Mwezi wa Mtoto wa Afrika mwezi Juni, ambao hutoa fursa kwa jamii kutafakari haki, ustawi na mustakabali wa watoto wa bara hili, Kampuni ya Barrick North Mara kupitia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara imeendelea kuonesha njia ya kuandaa mustakabali bora wa watoto kwa kuhakikisha wanapata elimu katika mazingira salama na yenye ubora.

Katika kutekeleza dhamira hiyo, tangu mwaka 2019 Barrick imewekeza shilingi bilioni 26.9 katika miradi 255 ya maendeleo ya jamii kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo. Kati ya fedha hizo, asilimia 35 sawa na shilingi bilioni 9.4 zimeelekezwa moja kwa moja katika sekta ya elimu.

Katika eneo ambalo utoro wa shule ulikuwa changamoto kubwa, viwango vya kuacha shule vilikuwa juu na wasichana wakikabiliwa na mazingira magumu zaidi katika safari yao ya elimu, huku walimu wakikumbwa na changamoto za makazi, uwekezaji wa Barrick North Mara umeleta matumaini makubwa kwa jamii.

“Kipimo cha kweli cha mafanikio yetu hakipo katika kiasi cha dhahabu tunachochimba, bali katika mustakabali tunaoujenga kwa watoto hawa ambao ndiyo nguvu kazi na tumaini la taifa letu,” amesema Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru, Juma Kengoe, ambaye kijiji chake ni miongoni mwa vinavyonufaika na mgao wa asilimia moja ya mapato ya mrabaha kutoka mgodini.

Katika mwaka 2025 pekee, Barrick ilikamilisha miradi 25 katika shule za msingi na miradi mingine 26 katika shule za sekondari zinazozunguka mgodi huo. Miradi hiyo ilihusisha ujenzi wa madarasa ya kisasa yaliyochukua nafasi ya miundombinu chakavu na isiyotosheleza mahitaji, hali iliyokuwa ikisababisha msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani.

Aidha, ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi wa kike unaendelea kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wasichana katika kupata elimu.

Miradi hiyo pia imejumuisha ujenzi wa nyumba za walimu, hatua inayolenga kuwapatia mazingira bora ya kuishi na kufanya kazi ili waweze kutoa elimu yenye ubora unaostahili kwa wanafunzi.

Vilevile, Barrick imechangia utengenezaji wa madawati, meza na viti vya walimu, pamoja na usambazaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuboresha miundombinu ya maji katika shule mbalimbali.

Mwalimu John Mwita, ambaye amefundisha katika Wilaya ya Tarime kwa zaidi ya miaka 15, amesema mazingira ya elimu yamebadilika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji huo.

“Kulikuwa na nyakati ambapo tulifundisha chini ya miti. Mvua iliponyesha, masomo yalisimama. Leo tuna madarasa yenye kuta, paa na hata umeme katika baadhi ya shule. Watoto wetu sasa wanajifunza katika mazingira yenye hadhi na heshima,” amesema.

Mbali na uwekezaji katika miundombinu ya elimu, Barrick imekwenda hatua zaidi kupitia mpango wa Friends of North Mara unaotekelezwa katika shule 10 za sekondari zinazozunguka mgodi huo.

Kupitia matamasha, semina na programu mbalimbali za mafunzo, mpango huo unawajengea wanafunzi ujuzi wa maisha na stadi laini (soft skills) ambazo mara nyingi hazipewi nafasi kubwa katika mfumo wa kawaida wa elimu.

Mafunzo hayo yanahusisha elimu ya fedha na uwekezaji, yanayowawezesha vijana kujifunza kuhusu kuweka akiba, kuwekeza na kutambua fursa za kiuchumi ili waweze kuwa wabunifu wa ajira badala ya kutegemea kuajiriwa pekee. Pia wanapatiwa elimu ya utunzaji wa mazingira, kampeni za kupinga ukeketaji pamoja na elimu ya haki za binadamu ili kuwajengea uwezo wa kujitambua, kujilinda na kusimamia haki zao.

“Nimetambua kwamba elimu siyo tu kufaulu mitihani. Ni kuhusu kutuandaa kwa maisha, kutusaidia kufanya maamuzi sahihi, kujilinda na kuwa raia wenye mchango chanya katika jamii,” amesema Neema Samweli, mmoja wa wanufaika wa mpango wa Friends of North Mara.

Kwa Grace Peter, mwenye umri wa miaka 17 na mwanafunzi wa kidato cha nne katika moja ya shule zinazoshiriki kwenye mpango huo, mafunzo hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha mabadiliko katika maisha yake.

“Kabla sikujua chochote kuhusu kuweka akiba wala haki zangu kama msichana. Sasa nawafundisha hata dada zangu wadogo yale niliyojifunza. Ndoto yangu ni kuwa wakili ili niweze kutetea na kulinda haki za wasichana wengine,” amesema Grace Peter.