Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa nchini ili kuongeza uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa, kufuatia kuongezeka kwa matukio yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na vihatarishi vingine vya asili na kijamii.
Hayo yameelezwa leo Juni 18, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, wakati akifungua Kikao cha Jukwaa la Taifa la Wadau wa Usimamizi wa Maafa kilicholenga kupitia na kuthibitisha Mwongozo wa Urejeshaji Hali Baada ya Maafa, Mwongozo wa Uendeshaji na Uratibu wa Uhawilishaji Fedha kwa Walioathirika wa Maafa, pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Maafa (DMIS).
Brigedia Jenerali Ndagala amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imekumbwa na matukio mbalimbali ya maafa yakiwemo mafuriko, ukame, maporomoko ya ardhi, upepo mkali, magonjwa ya mlipuko na ajali mbalimbali, hali ambayo imeathiri maisha ya wananchi, miundombinu, mazingira na shughuli za kiuchumi.
“Kwa kuzingatia hali hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha sera, mifumo, mikakati, mipango na nyenzo mbalimbali za usimamizi wa maafa ili kuhakikisha hatua zote za kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa zinafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022,” amesema.
Amesema kikao hicho ni hatua muhimu katika kuimarisha uratibu wa kitaifa wa usimamizi wa maafa kwa kuwa kinahusisha uthibitishaji wa nyenzo tatu muhimu zitakazochangia uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi wakati wa maafa na baada ya maafa.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Ndagala, Mwongozo wa Urejeshaji Hali Baada ya Maafa utaweka mfumo wa pamoja wa kitaifa wa kupanga na kuratibu shughuli za urejeshaji baada ya maafa, huku Mwongozo wa Uhawilishaji Fedha kwa Walioathirika wa Maafa ukiboresha utaratibu wa utoaji wa misaada ya fedha kwa waathirika. Aidha, Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Maafa (DMIS) utaimarisha ukusanyaji, uchambuzi, uhifadhi na matumizi ya taarifa za maafa kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
“Nyenzo hizi zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 kwa kuimarisha usimamizi wa taarifa, uratibu wa wadau, utoaji wa misaada na shughuli za urejeshaji hali baada ya maafa. Vilevile, zinachangia utekelezaji wa Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Hatari za Maafa kwa kuimarisha uelewa wa hatari za maafa, usimamizi wa vihatarishi, uwekezaji katika ustahimilivu na kuimarisha hatua za kujiandaa na kujenga upya kwa ubora zaidi baada ya maafa,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika sekta ya usimamizi wa maafa nchini yanatokana na ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, mashirika ya Umoja wa Mataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Judith Bihondwa, amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na maafa pamoja na kujenga ustahimilivu dhidi ya majanga mbalimbali.
Amesema ushirikiano huo utaendelea kulenga kuimarisha mifumo ya maandalizi, mwitikio na urejeshaji hali baada ya maafa kwa kuzingatia makundi yote ya jamii, hususan watoto na watu walio katika mazingira hatarishi.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa usimamizi wa maafa kutoka taasisi za Serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili na kuthibitisha nyenzo zitakazochangia kuimarisha usimamizi wa maafa na kuongeza ustahimilivu wa jamii nchini.

